Mtayarishaji Mwandamizi wa Vipindi vya Televisheni wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jeff Shellembi (kulia) akimwonesha Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla (kushoto) kaseti za kurekodi habari na vipindi mbalimbali yenye rangi nyekundu na bluu iliyo chini ya kiwango ambayo hudumu kwa miezi mitatu na kuathiri utendaji kazi wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo iliyofanyika leo kwenye kituo hicho cha televisheni cha TBC, Mikocheni jijini Dares Salaam . Wa pili (kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Joe Rugarabamu na aliyevaa kitenge ni Mkurugenzi wa Habari na Matukio wa TBC, Suzan Mungy.
Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla (katikati) akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC), Wilfred Nyachia baada ya kumaliza ziara yake katika shirika hilo na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Joe Rugarabamu.
Fundi Mitambo wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ally Kagomba (kushoto) akimwonesha Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, mitambo ya kurushia vipindi mbalimbali wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara kwenye kituo cha televisheni cha TBC,leo Mikocheni jijini Dares Salaam.
Waziri Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla (katikati) akizungumza na wajumbe wa Bodi na uongozi wa Shirika la Utangazaji Tanzania( TBC), mara baada kumaliza ziara yake katika shirika hilo. PICHA ZOTE NA MAGRETH KINABO – MAELEZO.
********************
Na Concilia Niyibitanga na Magreth Kinabo – HABARI
NAIBU Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Amos Makalla ameitaka Menejimenti ya Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) na Bodi yake kushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitendeakazi.
Mhe. Makalla ameyasema hayo leo (jana) wakati akizungumza na Menejimenti ya TBC na Bodi yake katika ofisi za kituo Televisheni ya Taifa (TBC1) cha Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Waziri Makalla ameiagiza Menejimenti ya Shirika hilo kutengeneza Mpango Mkakati wa kukabiliana na changamoto pamoja na matatizo ya Shirika hilo kwa kuzingatia vipaumbele na kuishauri Bodi ya shirika kuutumia mpango huo.
‘Tengenezeni Mpango Mkakati wa namna ya kutatua matatizo yanayolikabili Shirika, ili mtoe ushauri kwa Bodi’. Amesema Makalla.
Aidha, Makalla amekiri kuwa amejionea matatizo na kuzisikia changamoto zilizopo TBC na ameahidi kuwa Serikali iko bega kwa bega na Shirika hilo ili kuhahikisha kuwa matatizo hayo na changamoto hizo zinapatiwa Ufumbuzi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TBC, Bw. Joe Rugarabamu amesema, TBC inajitahidi kutekeleza majukumu yake ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii ya Watanzania pamoja na changamoto ya uwezo mdogo wa kifedha, gharama kubwa za kukusanya habari, kuzihariri na kuzisambaza kwa Watanzania wote.
Amesema kuwa, Shirika linakabiliwa na tatizo la uchakavu wa mitambo, gharama kubwa za upanuzi wa usikivu nchi nzima, uendeshaji wa mitambo hasa ukizingatia kupanda kwa gahrama za umeme na mafuta na malipo ya wafanyakazi zaidi ya 600.
Bw. Rugarabamu ameongeza kuwa, Shirika halina jengo moja la kuweka Ofisi za Radio na Televisheni pamoja hali inayofanya kuwa na sehemu ya Radio, huko Barabara ya Nyerere na Sehemu ya Televisheni, Mikocheni hivyo kusababisha gharama za uendeshaji kuwa kubwa.
Naye Mtayarishaji Vipindi Mwandamizi wa TBC, Bw. Jeff Shellembi amesema, TBC1 inakabiliwa na uhaba wa kaseti za kisasa kwa ajili ya habari za vipindi vya televisheni , hivyo kujikuta wakitumia kaseti zilizo chini ya kiwango hali inayosababisha kaseti hizo kuharibu deki na kuuwa kamera.
Bw. Ali Kagomba ni Fundi Mitambo wa TBC naye ameeleza kuwa, mitambo mingi ya Shirika hilo ya kurushia matangazo ni chakavu na mingine ni mibovu kabisa ikizingatia kuwa imeshapitisha muda wake wa kutumika.
“Kwa Kitaalam na kiufundi mitambo inatakiwa kutumika kwa miaka si zaidi ya 8, lakini mitambo yetu ina miaka zaidi ya kumi na huathiri ubora wa matangazo.” Amesema Bw. Kagomba.
Hii ni mara ya kwanza kwa Naibu Waziri, Mhe. Makalla kufanya ziara ya kikazi katika Shirika la TBC mara baada ya kuteuliwa kuwa Naibu wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
No comments:
Post a Comment