Habari za Punde

*HUDUMA ZA M-PESA NA TIGO PESA ZIMEGEUKA BENKI KAMILI, AU KARAA KWA WATEJA?

Mhudumu wa Wakala wa huduma ya Tigo Pesa wa mkoani Dodoma, ambaye hakuweza kufahamika jina lake, akimjibu hovyo mteja wake aliyefika mezani kwake kupatiwa huduma ya Tigo pesa hivi karibuni mjini Dodoma na kutokea kutoelewana baina yao kutokana na mabadiliko ya huduma hiyo.
*******************************
HUDUMA za kuweka na kutuma pesa kwa ndugu jamaa na marafiki, kupitia huduma za simu za mkononi, Tigo Pesa, M-pesa na nyinginezo, kwa kiasi flani zilikuwa tayari zimerahisishwa na mitandao hiyo, zilizojisajili kwa ajili ya kurahisisha kutoa huduma hiyo, ambayo kwa hakika imekwishajipatia umaarufu mkubwa tu na hasa pale mteja anapokwepa hadha ya kusimama katika foleni kubwa ya kusubiri huduma katika mabenki.

Lakini kwa sasa huduma hiyo iliyokuwa ikikimbiliwa na watu wengi kwa hivi sasa imegeuka kuwa karaa kubwa kwa wateja wake na hasa pale ilipoanzisha utaratibu ambao dhahiri ni ule unaofanana na wa kibenki ambao watu wengi walikuwa wakiukimbia na kuamua kurahisha kazi.

Baadhi ya huduma hizo zimekuwa zikimtaka mteja ili kujisajili lazima awe na picha kadhaa, barua ya Serikali ya Mtaa na Kitambulisho cha kupigia kura ama cha kazi huku pia kukiwa na mrorongo mrefu wa mambo yanayohitajika ili kukamilisha zoezi hilo.

Mbali na usumbufu huo, pia hivia sasa mitandao hiyo imeanzasha utaratibu 'eti' anayetaka kumtumia pesa hawezi kufika na kupata huduma hiyo katika ofisi ama meza ya Wakala wa huduma hiyo, hadi kwanza aweke katika simu yake na atume mwenyewe.

Inamaana Wakala hawa wamewekwa kwa ajili ya kuwawekea fedha wateja katika simu zao tu na si kwa kutoa huduma ya kutuma pesa, na hii inaonekana imewekwa ili mteja aweze kukatwa alimia kadhaa na si wakala anayetoa huduma hiyo kukatwa, sasa nini maana ya huduma hizi?

Ifikie mahali sasa Mawakala na watoaji wa huduma hizi walipie kodi inayolingana na ile ya kibenki kwani kila mteja anayetumia huduma hiyo hukatwa fedha kulingana na pesa anayotuma je, ni watanzania wangapi hutumia huduma hizi kwa siku? na Makampuni haya huingia kiasi gani kwa siku kupitia mawakala wao wanaotoa huduma hizi?

Kwa kweli hivi sasa huduma hizi zimegeuka kuwa usumbufu badala ya kuwa rahisi.

Mtandao huu wa sufianimafoto, umelazimika kuandika makala hii fupi baada ya kukutana na tukio hili la usumbufu na kushuhudia jamaa mmoja akilalamika wakati akipandishiwa kwa lugha isiyofaa na mtoa huduma hii (Pichani katikati juu). Ambapo mteja alifika meza hii kwa lengo la kumtumia nduguye pesa kiasi cha Sh. 300,000/= ambaye alikuwa njiani akisafirishwa kutokana na ugonjwa.

Jamaa huyu bila kujua kuwa huduma hizo zimebadilishwa mfumo mzima wa kutuma pesa, alifika na kumtaka mtoa huduma huyo, kumtumia pesa hizo kwa namba ambayo alimpatia na akafanya kama alivyotakiwa, lakini baada ya mtoa huduma huyo kumaliza kazi yake hiyo, alijaribu kuibipu namba aliyoitumia na kusikia ikiita kwingine na si mahala hapo, kwani alitarajia ingeita mfukoni kwa jamaa huyo aliyempa pesa hizo kutuma.

Baada ya kusikia ikiita mahala pengine, mdada huyo alianza kuwaka na kumkaripia mteja wake huyo, ''We unajifanya mjanja, hata me ni mjanja zaidi yako, unataka mie ndo nikatwe hiyo kamisheni hapa umeingia choo cha kike, naenda kuiblock hiyo namba na huwezi kuto pesa hiyo wala kuipata leo'' alisema mdada huyo

Mteja huyo alipojaribu kuhoji kutolewa maneno makali kama hayo bila kufahamishwa kinachoendelea, ndiyo mtoa huduma kama hiyo wa mtandao mwingine aliyekuwa pembeni ya mdada huyo mkali, alianza kumfafanulia mteja huyo asiye wake, juu ya mabadiliko ya huduma hiyo na nini kinatokea baada ya kufanya kama ilivyokwishafanywa, ambapo mteja alielewa na kumshangaa mtoa hudua ambaye hakutaka kumfahamisha kutokana na yeye hakuwa akijua kuwa siku hizi Wakala, hatumi pesa kwa mteja bali anaweka pesa kwa mteja tena aliyefika mahala hapo akiwa na simu yake.

Alipouliza kuhusu kurejeshewa fedha zake baada ya kuziblock, mdada huyo aliwaka tena, ''mi siwezi kutoa pesa zangu nikakupa wewe labda usubiri mpaka kesha zikisharudishwa ndo uje uchukue kwa sababu ulitaka kunifanyia uhuni,'', alisema mdada huyo.

''Sasa kama hizo pesa zitarudishwa kwako na mie sitakuwepo ni msafiri wewe si unirudishie pesa zangu kisha wewe utachukua hizo kwani tayari umeshaziblock mie siwezi kuzitoa wala kuzipata?'' alihoji mteja

''Aah, hiyo kazi sifanyi wewe hata kama unasafiri nenda kesho urudi kuchukua'', mdada huyo aliendelea na msimamo wake hadi alipoingilia kati tena mtoa huduma kama hiyo wa pembeni yake, alipomwelekeza mwenzake kuwa, mteja aache namba yake ili zitakaporudi amtumie katika simu yake, ndipo ukafikiwa muafaka mteja akiondoka mahala hapo bila kupata huduma huku mgonjwa wake akiendelea kuteseka hadi kesho yake mzigo utakaporejeshwa kwake ili amtumie tena. Sasa hii raha au karaha???? 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.