Habari za Punde

*RAIS WA MADAKTARI AFIKISHWA MAHAKAMA YA KISUTU LEO KWA TUHUMA ZA KUHAMASISHA MGOMO WA MADAKTARI

Dkt. Mkopi (kushoto) akisindikizwa kuingia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, kujibu tuhuma zinazomkabili kuhusu mgomo wa Madaktari.
**********************************

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),  Dkt. Mkopi,  leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kusomewa mashtaka mawili yanayomkabili juu ya mgomo wa madaktari, ambapo baadaye aliachiwa kwa dhamana.

Akisomewa mashitaka hayo Mahakamani hapo, Mkopi, alielezwa kuwa ameshitakiwa kwa makosa mawili ya kupuuza amri halali ya kusitisha mgomo na jingine ni la kuhamasisha mgomo huo.

Ilidaiwa mbele ya Hakimu Faisal Kahamba, kuwa kati ya Juni 26 na Juni 28 mwaka huu, Mkopi, alipuuza amri halali ya Mahakama Kuu (Divisheni ya Kazi), ya kuzuia mgomo wa madaktari na  badala yake kuhamasisha kuendelea kwa mgomo huo kinyume cha sheria. 

Rais huyo wa MAT,baada ya kusomewa mashitaka hayo,  alichiwa kwa dhamana na Hakimu Kahamba, baada ya kutimiza masharti ya dhamana, ambayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili waliomdhamini kwa Sh. 500,000 kila mmoja.

Kesi hiyo ilivuta hisia za watu wengi ambapo mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, walifurika mahakamani hapo, wakiwemo madaktari walioonekana kumuunga mkono rais wao. Habari na Picha kwa hisani na Mtandao wa Straika

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.