Habari za Punde

*RISALA YA YA MWZI MTUKUFU WA RAMADHAN YA MHE. RAIS WA ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein,akitoa Risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, kwa  wananchi na kuwataka kufanya Ibada kwa Bidii,hata hivyo Mhe, Rais aliwakumbusha wananchi kufanya mambo muhimu yaliyowajibu kufanywa katika mwezi huu ili kufanikiwa hapa Duniani na kesho Akhera twendako. Picha na Ramadhan Othman,Ikulu
********************************************
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa misingi ya kutodhulumiana katika bei, viwango na vipimo hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akisoma risala ya Ramadhani  kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa mwaka huu wa 1433 Hijriya sawa na mwaka 2012 Miladia.

Katika maelezo yake Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni wa neema kibiashara lakini ni vyema kufanya neema hiyo iwe kwa wauzaji na kwa wanunuzi.

Alieleza kuwa Muuzaji anauza bidhaa zake nyingi  zaidi kwa hivyo anapaswa kuhakikisha zina ubora na anachuma faida kwa kiasi ya anachouza.

Aidha, alisema kuwa mnunuzi naye anahitaji kupewa bei iliyo nafuu hasa kwa bidhaa ambayo Serikali imeipunguza kodi, kwani Serikali kama kawaida itapunguza ushuru kwa biadhaa muhimu za chakula ili kuwawezesha wananchi kupata unafuu wa bei.

“Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa wanasafirisha bidhaa kama vile unga, sukari na mchele walizotozwa kodi ya chini na kuzisafirisha kwa njia ya magendo nje ya Zanzibar ili wapate faida kubwa’,alisema Alhaj Dk. Shein.

Kutokana na mambo hayo Alhaj Dk. Shein alisema kuwa husababisha upungufu wa baadhi ya vyakula na kuwasababishia shida wananchi wakati huu  wa mwezi wa Ramadhani.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa shukurani kwa wakulima nchini kwa kujiandaa kuwaopa huduma nzuri wananchi hasa katika upatikanaji wa chakula kwa ajili  ya futari huku akieleza kuwa serikali imeweka mazingira mazuri ya biashara hasa katika Mwezi huo wa Ramadhani.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nayo itajitahidi kufanya kila linalowezekana ili kuwasaidia wananchi katika kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo mbali mbali nchini.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali imo katika juhudi za kuwaandalia wananchi wake maisha bora, kwa kupitia mageuzi ya katiba na pia kwa kuhesabiwa watu, mambo ambayo yamo katika sheria.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu rehema,na kujaalia subira huku akielezea juu ya tukio la kuzama kwa meli ya MV SKAGIT ambapo alieleza kuwa tayari maiti nyengine 22 tokea asubuhi ya leo hadi anatoa risala yake tayari zimeokolewa.

Alhaj Dk. Shein pia, alitoa wito kwa wananchi kuwa watendaji wema na hisani baina yao na hasa kwa masikini na wasiojiweza ambapo utoaji sadaka ni jambo la msingi na hakuna budi kulizingatia zaidi katika mwezi huo wa Ramadhan ili wale wenye kipato cha chini nao uwe ni mwezi wa furaha kwao.

Alisema kuwa kwa kuwa Ramadhani mwaka huu imekuja katika msimu wa Watalii na ziara za Wazanzibari wanaoishi nchi za nje, inapaswa kwa umoja wao kuonesha wema wao na mambo mema kwao na kudumisha sifa ya
ustaarabu, uvumilivu, mshikamano na kuelimishan kwa upole kwa yale wasiyoyajua ya mila za Kizanzibari.

Aidha aliwataka wananchi wasiowajibika na saumu kama kawaida watoe ushirikiano na wawe wastahamilivu kwa wenzano wanaofunga na wajitahidi kutumia fursa hiyo vyema bila ya kuwakirihisha wengine.

Alhaj Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulizni wa watu na mali zao kwa kushirikiana na vijana wa ulinzi shirikishi ili wananchi wapate utulivu na watekeleze
saumu kwa amani.

Dk. Shein aliwataka wazazi na walezi nao kuzisimamia vyema nyendo za watoto wao katika mwezi huo na kuwahimiza zaidi katika ibada na darsa. Pia, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kuutumia muda mwingi kuisoma na
kupata maarifa ya Qur-an katika Mwezi huu wa Ramadhan, mafunzo ambayo yatadumi siku zote.

Wakati huo huo, viongozi kadhaa walifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumpa pole Dk. Shein pamoja na wananchi kwa ujumla kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV SKAGIT na kusababisha vifo pamoja na majeruhi. Miongoni mwa  viongozi hao ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Kharib Bilal pamoja na ujumbe wa Wabunge 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Shamsi Vuai Nahodha. 


Imetolewa na Rajab Mkasaba
IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.