Na Mwandishi wetu, Renton, Washington
Timu ya Seattle Sounders FC imetangaza ushirikiano na Tanzania, nchi ambayo ni nchi kubwa kabisa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.Ushirikiano huo ulitiwa saini na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Balozi Hamis Kagasheki (Mbunge) na Mmiliki wa timu ya Seattle Sounders Joe Roth katika hafla fupi iliyofanyika jana mjini Renton.
Mbali ya Waziri Kagasheki, wengine walioshuhudia kutiwa saini kwa ushirikiano huo ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mheshimiwa Balozi Mwanaidi S. Maajar, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania Dr. Aloyce Nzuki na maofisa wengine kutoka Wizara ya Utalii, Ubalozini na maofisa wa Seattle Sounders FC.
Mambo muhimu katika ushirikiano huo ni uwekwaji wa alama za vivutio vya utalii vya Tanzania katika maeneo mbali mbali kama CenturyLink Field na Starfire Sports Complex, uwanja wa mazoezi wa Sounders FC uliopo eneo la Tukwila.
"Ushirikiano wetu na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) utasaidia kutangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania nje ya mipaka yake kwani kuna vivutio vya ajabu mno na kuleta unafuu kwa watalii ,” alisema Mmiliki wa timu ya Sounders FC, Joe Roth. Na kuongeza kuwa ushirikiano huo utatoa nafasi muhimu kwa soko la Utalii wa Tanzania nchi ya mipaka yake.
Waziri Kagasheki mbali ya kupongeza kwa kufanikisha hatua hiyo muhimu katika sekta ya Utalii nchini alisema kuwa ushirikiano huo utatoa fursa nyingi kwa Watanzania na Wamerekani kwani utahimarisha juhudi za Wizara ya Utalii katika kukuza soko la Utalii wa Kimataifa na wa Ndani.
Mheshimiwa Kagasheki pia alisema kuwa ushirikiano huo utatoa fursa za kibiashara kwa nchi zote mbili na kuongeza uwekezaji.
Katika kuhakikisha zoezi ujumbe wa kupromoti vivutio vya Utalii wa Tanzania vinawafikia wengi, michoro mbali mbali ya ukutani itachorwa kwenye ndani ya uwanja upande wa Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki na itaonekana kwa mara ya kwanza kwenye televisheni nchini Marekani wakati wa mechi ya Sounders FC dhidi ya timu ya Chelsea katika uwanja wa Field CenturyLink Julai 18 (Tanzania Julai 19).
Pia maofisi wa TTB watakuwa mbele wakati wa mkutano wa kabla ya mechi wa mashabiki wa soka na kuzungumzia masuala mbali mbali ya utalii na usafiri katika nchi yao.
Timu ya Seattle Sounders FC ilianza majadiliano ya ushirikiano na Tanzania mwaka 2010 ambapo kocha msaidizi wa timu hiyo Kurt Schmid alisafiri kuja nchini katika mpango wa kutafuta vipaji vya wachezaji.
Mchezaji wa timu ya Taifa, Mrisho Ngassa kutoka timu ya Azam FC alisafiri mpaka Marekani na kucheza mechi ya kihistoria kati ya Seattle Sounders na timu ya Machester United mwaka jana (2011).
No comments:
Post a Comment