Mwenyekiti wa Kijiji cha Emairete, Moran Poyoni, akimkabidhi zawadi ya fimbo maalumu Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Samsung, Choi Woo-Soo, wakati wa hafla ya kukabidhi madarasa kwa shule ya Irmorijo, yaliyokarabatiwa na Kampuni ya Samsung na kutangaza msaada wa milioni 144 kwa shule hiyo na Sekondari ya Winning Sprit Monduli Arusha jana.
Mama wa Kimasai akimpa zawadi Dada wa Kikorea wakati wa hafla ya kukabidhi madarasa kwa shule ya Irmorijo baada ya ukarabati uliofanywa na Kampuni ya Samsung na kutangaza msaada wa Sh. milioni 144 kwa shule hiyo na Sekondari ya Winning Sprit Monduli Arusha jana.
Makamu wa Rais wa Samsung, Choi Woo-Soo (katikati), Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Joika Kasunga na Diwani wa Kata ya Monduli juu, Bariki Sumuni wakishangilia baada ya kukata utepe kwa pamoja kuashira uzinduzi wa madarasa ya Shule ya Msingi ya Irmorijo Monduli Arusha, yaliyokarabatiwa na Kampuni ya Samsung na kuzinduliwa rasmi jana.
Wakinamama wa Kimasai wa Kijiji cha Emairete Wilayani Monduli, wakimkabidhi zawadi ya Mbuzi, Makamu wa Rais wa Samsung, Choi Woo-Soo wakati wa hafla ya kukabidhi madarasa kwa shule ya Irmorijo.
Makamu wa Rais wa Samsung, Choi Woo-Soo akiwa katika vazi la Kimasai huku akionyesha zawadi ya fimbo maalum aliyokabidhiwa wakati wa hafla ya kukabidhi madarasa kwa shule ya Irmorij.
**************************
Na Mwandishi Wetu, Arusha
KITENGO cha biashara na ufumbuzi cha kampuni ya Samsung Electronics kimetangaza mpango wa msaada wa shilingi za kitanzania milioni 144 sawa na dola za Kimarekani 90,000 kwa ajili ya kusaidia shule ya msingi Ilmorijo na shule ya sekondari ya Winning Spirit za Wilaya ya Monduli jijini Arusha.
Makamu wa Rais wa Samsung Bw. Choi Woo-Soo alisema kuwa hii ni sehemu tu ya mpango endelevu wa kusaidia jamii wa kampuni ya Samsung Electronics kuwekeza katika elimu ndani ya nchi za Afrika.
“Sekta ya elimu ni kipaumbele kikubwa kwetu kama Samsung na tutaendelea kuwekeza katika sekta hii nchini Tanzania na bara la afrika kwa ujumla kwa sababu bila ya elimu nchi haiwezi kupata maendeleo ya kiuchumi na viongozi bora na sio bora viongozi,” alisisitiza makamu wa Rais wa kampuni ya Samsung Wilaya ya Monduli, jijini arusha wiki hii.
Kampuni ya Samsung ilikabidhi nyumba mbili za walimu zenye uwezo wa kukaa familia nne za walimu na madarasa manne ya shule ya Msingi ya Ilmorijo.
Shule hiyo itapata msaada wa kitaaluma na pia matengenezo ya majengo. Hii inajumuisha baadhi ya wanafunzi kulipiwa gharama za shule, kuongezeka kwa idadi ya walimu shuleni, kuongezeka kwa madarasa ya masomo ya ziada, ushauri nasaha kwa familia na mipango mbalimbali ya elimu ya afya.
Bw Woo-Soo alifafanua kuwa Samsung itakuwa ikifanya matengenezo na kurekebisha huduma mbalimbali shuleni, fenicha na vifaa vingine pamoja na kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana kilichoboreshwa zaidi.
Kwa mujibu wa afisa huyo, shule ya kuendeleza vipaji vya michezo ya watoto ya Winning Spirit iliyoko jijini Arusha itapata nafasi ya kutoa mwanafunzi mmoja ambaye atalipiwa gharama za masomo na kupewa mafunzo ya riadha.
Mkakati huu utasaidia kuunda watoto wenye vipaji ambao watapata usaidizi wa kampuni ya Samsung na kuwa wanamichezo bora nchini na duniani.
“Tumejizatiti kuweka tofauti ya wazi kabisa katika maeneo ambayo wateja wetu wanaishi” alisema Bw. Woo-Soo.
Aliogeza kuwa huu ni uthibitisho wa miradi waliyoianzisha katika maeneo mengi ya bara la Afrika katika sekta ya elimu, kuunganisha vijiji na mahitaji ya kimsingi ya jamii.
Mipango ya kuitumikia jamii inayofanywa na kampuni ya Samsung katika bara la Afrika inalenga kujenga miradi endelevu inayofikia mahitaji halisi ya jamii husika kwa kuzingatia uchumi wao, asisitiza Bw. Woo-Soo.
Mradi unaoaminika zaidi katika mpango huu ni Samsung Electronics Engineering Academy, huu umetekelezwa kukidhi haja ya kuendeleza mafundi wenye ujuzi ambao watakuwa watoa huduma bora waliowezeshwa ili kuzalisha mali na kuinua uchumi.
Mradi wa programu hii umeanzishwa katika nchi za Afrika ya Kusini, Kenya na Nigeria kwa lengo la kutatua tatizo la upungufu wa wataalamu na mafundi katika Afrika kwa kutoa mafunzo ya ufundi kwa vitendo kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Katika programu hii wanafunzi wanapatiwa mpango wa masomo ya ufundi kwa mwaka mmoja, mafunzo haya hujumuishwa katika mitaala ya masomo ya ufundi.
Miradi ya elimu ya kampuni ya Samsung pamoja na mipango ya wafanyakazi kujitolea ni sehemu ya lengo kuu la kampuni hii inagusa moja kwa moja maisha ya watu milioni tano katika bara la Afrika kufikia mwaka 2015.
“Tunaunganisha uwezo wetu katika ubunifu ili kubadilisha jamii na maisha kuwa bora zaidi, kutunza sayari yetu kwa ajili ya vizazi vijavyo na kufungua nafasi za mafanikio kwa watu,” alinena kiongozi huyo wa Samsung.
Mipango ya kuitumikia jamii ya kampuni ya Samsung katika bara la Afrika inaendana na mpango wa global ‘Hope for Children’ initiative, ambao unafanya dunia kuona haja ya kuboresha elimu na afya ya watoto katika jitihada za kuboresha maisha ya watu na jamii.
No comments:
Post a Comment