MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba SC jana walihitimisha Wiki ya Simba na Jamii, kwa kutoa misaada yenye thamani ya Sh. Milioni 1.5 katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Maunga Orphanage Center, kilichopo Kinondoni Hananasif, Dar es Salaam.
Baadhi ya wachezaji wa Simba, Emanuel Okwi, Juma Nyosso, Uhuru Suleiman, Meneja Nico Nyagawa, Daktari Cossmas Kapinga, Ofisa Habari, Ezekiel Kamwaga, Katibu Evodius Mtawala na Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ walijumuika na watoto wa kituo hicho na kuwafariji kwa zawadi.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo na fedha taslimu Sh. 500,000, Kaburu alisema kuwa huo ni mwanzo tu na watakuwa wakiendelea na utaratibu huo wa kusaidia kituo hicho na vinginevyo.
“Simba SC ni taasisi kubwa na tumeguswa na kilio chenu, nasi tunaahidi kuendelea kusaidia kadri ambavyo tutakuwa tukipokea maombi kutoka kwenu,”alisema Kaburu.
Akitoa shukrani baada ya kupokea misaada hiyo, Katibu wa kituo hicho, Rashid Mpinda, aliwashukuru Simba SC na kuwatakia kila la heri katika msimu ujao, kuanzia kwenye Ligi Kuu na michuano ya Afrika.
Maunga Orphanage Center kilianzishwa mwaka 2008 kikiwa na watoto wanne, chini ya mmiliki wake, Mama Zainab Bakari na sasa kina watoto zaidi ya 60, kati ya hao 30 wakiwa wanaishi moja kwa moja kituoni hapo na 30 wengine wanashinda kituoni na kwenda kulala kwa walezi wao.
Mama Zainab alisema kwamba changamoto zinazowakabili mbali na kukosa eneo la kutosha kwa malazi ya watoto na hata eneo la kufanyia michezo, lakini pia gharama za kuwasomesha watoto hao pia ni baadhi ya changamoto nyingine zinazowakabili.
Alisema watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule, wanawasomesha katika shule za Hananasif na Mkunguni na kinachowasumbua ni ada za watoto na michango mingine ya shule.
Mama Zainab alisema kituo chao hadi sasa hakina wafadhili, zaidi ya kutegemea michango ya wadau kama ambayo Simba SC wametoa leo na pia misaada ya Diwani wao, Abbas Tarimba.
Alisema wanahitaji eneo lingine kubwa kwa ajili ya kujenga kituo kikubwa kitakachopokea na kuhudumia watoto wengi zaidi, hivyo anaomba wajitokeze wafadhili wa kuwasaidia.
Emmnauel Okwi, Uhuru na Nyosso kama ilivyokuwa kwa viongozi wao, walionyesha kuguswa na matatizo ya watoto hao na kuahidi binafsi kutembelea tena katika kituo hicho kuwasaidia.
Katika ratiba ya Wiki ya Simba SC na Jamii, mambo mawili tu yameshindikana kufanyika, kutembelea shule ya Msingi Mgulani na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), ambao ni wadhamini wa klabu hiyo kupitia bia ya Kilimanjaro Premeum Lager.
Katika mfululizo wa Wiki ya Simba na Jamii, jana timu hiyo ilicheza mechi ya kirafiki na Nairobi City Stars ya Kenya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufungwa mabao 3-1 katika Simba Day.
Lakini kufungwa huko kwa Simba kulitokana na kocha Milovan Cirkovick kubadilisha karibu kikosi kizima kilichoanza na kuingiza wachezaji wapya kipindi cha pili, ambao waliitoa City Stars ya Nairobi nyuma kwa 1-0 na kuipa ushindi wa 3-1.
Simba ilitangulia kupata bao kupitia kwa Felix Sunzu dakika ya 15, pasi ya Mwinyi Kazimot na ilikwenda kupiumzika ikiwa mbele kwa bao hilo.
Lakini kipindi cha pili, kipa aliyempokea Juma Kaseja, Hamadi Waziri alitunguliwa mabao matatu katika dakika 57 na Duncan Owiti, dakika ya 64 na Bruno Okullu na dakika ya 79 na Boniphace Onyango.
Mapema katika tamasha hilo, Simba ilitoa tuzo mbalimbali kwa wachezaji wa sasa na wa zamani kwa mchango wao kwenye klabu hiyo, pamoja na baadhi ya wadau wake.
Waliopewa tuzo kwa wachezaji wa sasa, ni Shomary Kapombe (Nidhamu), Emmanuel Okwi (Mchezaji bora wa msimu) na marehemu Patrick Mfisango (Heshima).
Wa zamani ni Haidari Abeid ‘Muchacho’ (Mchezaji Bora miaka ya 1970), Hamisi Kilomoni (Mchezaji Bora Miaka ya 1960), Ally Sykes (Heshima, Udhamini), Profesa Philemon Sarungi (Mchango wa muda mrefu klabuni) na Gaorge Kavishe, Meneja wa Kilimanjaro Beer, Wadhamini wa sasa wa Simba SC.
Katika mechi ya kwanza, timu na wanawake ya Simba, Simba Queens mchana, iliifunga Ever Green ya Temeke mabao 5-3 katika mchezo wa Ligi ya Wanawake, Dar es Salaam uliokwenda sambamba na tamasha la Simba Day, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba alikuwa ni Maimuna Hamisi ‘Ronaldo’ aliyefunga mabao matatu, katika dakika za tano, 62 na 64, wakati mabao mengine ya Malkia wa Msimbazi, walio chini ya kocha Anthony Makunja, yalifungwa na Grace Tony dakika ya 48 na Neema Kuga dakika ya 59.
Mabao ya Ever Green yalifungwa na Sherida Boniface dakika ya 53, Vumilia Maarifa dakika ya 55 na Amina Siraj dakika ya 61.
WIKI YA SIMBA NA JAMII ILIVYOKUWA:
Agosti 5, 2012: Mkutano Mkuu wa mwaka Simba SC (Polisi Oystrebay)
Agosti 7, 2012: Kutembelea wagonjwa Mwananyamala hospitali
Agosti 8, 2012: Simba 1-3 Nairobi City Stars (Simba Day Uwanja wa Taifa)
Agosti 9, 2012: Kutembelea watoto yatima Maungu Orphanage Center
No comments:
Post a Comment