Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari leo, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Amezungumzia mambo kadhaa ikiwemo maandalizi ya uchaguzi mkuu wa CCM na kulaani matukio ya vurugu yaliyotokea Mbagala, Dar es Salaam. Picha na Bashir Nkoromo
************************************
Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika tarehe
13/10/2012 pamoja na mambo mengine kilipanga ratiba ya Mkutano Mkuu wa Taifa
iwe kama ifuatavyo:-
Mkutano Mkuu wa Nane wa Kawaida wa CCM utafanyika tarehe 10 – 12 Novemba,
2012 . Kwa kawaida Mikutano Mikuu ya CCM
imekuwa ikifanyika kwa siku mbili.
Lakini safari hii CCM imeamua mkutano huo uwe wa siku tatu ili kutoa
fursa kwa Wajumbe kujadili kwa kina taarifa muhimu zitakazowasilishwa.
Mkutano huo utafanyikia KIZOTA – Dodoma mahali ulipofanyika Mkutano Mkuu
uliopita mwaka 2010.
Shughuli muhimu zitakazofanywa wakati wa Mkutano huo zitakuwa:-
Kufanya marekebisho ya Katiba ya CCM ya 1977 toleo la 2010 kwa kuzingatia
mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa yatakayowasilishwa kwenye Mkutano huo.
Kupokea na kujadili taarifa mbalimbali zikihusu:-
Taarifa ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka
2007-2012 itakayowasilishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.
Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Shughuli za Uchaguzi ambazo zitahusu Uchaguzi wa:-
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Viti Kumi vya Bara na kumi vya
Zanzibar.
Mwenyekiti wa CCM.
Makamu wawili wa Mwenyekiti mmoja kutoka Bara na mwingine kutoka Zanzibar.
Shughuli za Mkutano Mkuu zitatanguliwa na kuweka Jiwe la Msingi la Majengo
ya Ukumbi wa Mikutano na Makao Makuu ya CCM eneo la Medelii katika Manispaa ya
Dodoma. Shughuli hii itafanywa na
Mwenyekiti wa CCM Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
MAANDALIZI YA MKUTANO
Shughuli za Maandalizi ya Mkutano zinaendelea vizuri. Shughuli hizi ni pamoja na uchapaji wa
Nyaraka mbalimbali; usafiri wa Wajumbe, Maandalizi ya Ukumbi na huduma nyingine
muhimu kwa ajili ya kufanikisha Mkutano huo.
VURUGU ZILIZOTOKEA MBAGALA
Chama cha Mapinduzi kimesikitishwa na matukio yaliyotokea Mbagala, jijini
Dar es Salaam, tarehe 11 Oktoba 2012. Chama cha Mapinduzi kinalaani kitendo cha
kukojolewa kwa kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislam, yaani Kuran. Vilevile,
Chama cha Mapinduzi kinalaani vitendo vya vurugu na kuvamiwa na kuchomwa moto
makanisa.
Vitendo vyote hivi havifanani na mila na desturi za Watanzania. Kitendo cha
kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu hakikubaliki. Na kitendo cha kuvamia
na kuchoma moto nyumba za ibada za Wakristo na kufanya vurugu pia hakikubaliki.
Tanzania ni nchi inayofahamika na kusifika kwa amani na utulivu na kwa umoja na
mshikamano wa watu wake wa kabila, rangi na dini zote. Chama cha Mapinduzi
kinawasihi wananchi wawe na subira na uvumilivu yanapotokea matukio kama haya
na waviachie vyombo vya dola vifanye kazi yake.
Ni imani ya CCM kwamba vyombo vya
dola vitachukua hatua stahiki kwa wote waliohusika na matukio haya. Pia,
tunatumaini kwamba hali ya amani na utulivu itarejea Mbagala kama kawaida.
UTEUZI WA MAJINA YA WAGOMBEA NAFASI MBALIMBALI
MKOANI KILIMANJARO
Kamati Kuu pia imefanya uteuzi wa mwisho wa majina ya Wanachama wa CCM
walioomba nafasi za Uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika nafasi za
Uenyekiti wa CCM Wilaya na Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nafasi ya Wilaya
za Siha na Moshi Vijijini.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM; uteuzi wa mwisho wa nafasi hizi hufanywa na
Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini Kikao cha tarehe 25/9/2012 kilichofanyika
Mjini Dodoma hakikufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi hizi katika Wilaya za
Siha na Moshi Vijijini. Hivyo, Kikao hicho kilikasimu madaraka yake ya uteuzi
kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Nafasi za Uongozi zinazogombewa na majina ya walioteuliwa ni kama
ifuatavyo:-
(1) Nafasi ya Mwenyekiti wa
CCM Wilaya ya Moshi Vijijini
Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni 13.
Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-
(a) Ndugu Shayo Isack EDWARD
(b) Ndugu Masenga John GABRIEL
(c) Ndugu Shao C. GEOFREY
(d) Ndugu Mallya Mathew MARTIN
(2) Nafasi ya Mwenyekiti wa
CCM Wilaya ya Siha
Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni wanne (4). Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-
(a) Ndugu Tawida Nahato BASSO
(b) Ndugu Simon Lekshon MOLLEL
(c) Ndugu Happiness Mathias MUNUO
(d) Ndugu Oscar Jeremiah TEMI
(3) Nafasi ya Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa Wilaya ya Siha
Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni saba (7). Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-
(a) Ndugu Meijo Loloinyo LAIZER
(b) Ndugu Joha Shabani MTAWAZO
(c) Ndugu Happiness Mathias MUNUO
(d) Ndugu Cosmas Sebastian MUSHI
Imetolewa na:
_
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
14/10/2012
No comments:
Post a Comment