Na Mwandishi Wetu, Arusha
MISS Dar City Center ambaye pia alishika nafasi ya pili katika shindano la Redd’s Miss ilala, Magdalena Roy amefanikiwa kuingia 15 Bora ya Redd’s Miss Tanzania baada ya juzi usiku kufanikiwa kutwaa taji la Top Model.
Magdalena anakuwa mshindi wa pili kuingia katika hatua hiyo, akiungana na Miss Mbulu, Lucye Stephano ambaye wiki iliyopita alitwaa taji la Miss Photogenic.
Katika shindano la Top Model lililofanyika kwenye hoteli ya Naura Spring, mjini hapa lilikuwa na upinzani mkali kutoka kwa washiriki wote wa Redd’s Miss Tanzania.
Mbali na Magdalena warembo wengine waliofanikiwa kuingia katika tano bora walikuwa ni Mary Chizi (Ilala), Irene Veda (Lindi), Belinda Mbogo (Dodoma) na Sina Revocatus (Elimu ya Juu).
Akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana, Afisa Habari wa Kamati ya Miss Tanzania, Haidan Ricco alisema warembo hao jana waliondoka kuelekea Tanga kwa ajili ya kutembelea mapango ya Amboni, kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Warembo wapatao 30 wanawania taji la Redd’s Miss Tanzania, ambalo kwa sasa linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original.
2 CASTLE LAGER SUPPER FAN
Wakali sita wa Castle Lager Superfans kujulikana leo
Na Mwandishi Wetu
WASHINDI sita wa shindano la kumsaka shabiki bora wa Ligi Kuu ya England, maarufu zaidi kwa jina la ‘Castle Lager Superfans’ wanatarajiwa kujulikana leo.
Shindano hilo linaendeshwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Castle Lager ambao pia ni wadhamini wenza wa Ligi Kuu ya England.
Meneja wa Bia ya Castle Lager, Kabula Nshimo alisema mchujo wa mashabiki hao ulikuwa mgumu kutokana na watu wengi kujitokeza.
Kabula alisema, jumla ya mashabiki 361 walijitokeza kwa kutuma picha zao katika mtandao wa kijamii wa Facebook na promosheni walizoziendesha katika mikoa mbalimbali.
Meneja huyo alisema, baada ya mchujo walipatikana washindi 32 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Shinyanga, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro, ambao walipigiwa kura na kupatikana 15.
“Katika hao 15 ndio ambao walifanyiwa mahojiano ya ana kwa ana , hivyo wamechujwa na kupatikana sita, ambapo watasakwa washindi wawili ili waunde timu ya Castle Lager Superfans Tanzania,” alisema.
Washindi hao sita watakaotangazwa leo wanatarajiwa kuzunguka nzima ili kuomba kura kutoka kwa mashabiki wa Ligi Kuu England.
Kabula alisema washindi hao wawili watakaopatikana, wataungana na wengine kutoka Swaziland, Zambia, Afrika Kusini na Zimbabwe ili kuunda timu ya ushangiliaji itakayogharamiwa kila kitu katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika hapo mwakani. Fainali hizo zitafanyika Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment