Habari za Punde

*SERIKALI YA ZANZIBAR YAAHIDI KUTOA USHIRIKIANO NA UNDP KATIKA KUDUMISHA USTAWI WA JAMII

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpongeza Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Alberic Kacou kufuatia Umoja wa Mataifa kutimiza Miaka 67 tokea kuasisiwa kwake. Pongezi hizo amezitoa Ofisini kwake katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa aliyepo Tanzania Bw. Alberic Kacou akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwakilishi Mpya wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa Zanzibar Bibi Anna Senga.Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bwana Alberic Kacaou na kushoto kwa Balozi Seif ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohd.
 ****************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Umoja wa Mataifa (UN) kwa kutimia miaka 67 tokea kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1945.

Balozi Seif ametoa pongezi hizo wakati akisalimiana na Ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) Ofisini kwake katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Ujumbe huo wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa ulioongozwa na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa aliyepo Nchini Tanzania Bw. Alberic Kacou uliambatana pia na Mwakilishi wa Shirika hilo aliyepo Zanzibar Bibi Anna Senga.

Balozi Seif amesema Umoja huo umeundwa maalum kwa lengo la kutoa huduma itakayokidhi mahitaji ya Mataifa yote Wanachama wa Umoja huo hasa katika masuala ya kustawisha Amani na ustawi wa Jamii.

Ameeleza kwamba Taasisi zilizoundwa chini ya mwavuli wa Umoja huo zimekuwa zikiendelea kutoa huduma mbali mbali kwa Mataifa Wanachama zilizopelekea kupiga hatua kubwa za Maendeleo hasa katika Nchi za Dunia ya Tatu.

Amesema Jamii za Kimataifa zimekuwa zikishuhudia ufanisi huo hasa katika miradi ya Afya, Chakula na lishe, Maji, sambamba na kudhamini Mafunzo ya Elimu ya Uraia kwa lengo la kutandika Demokrasia Duniani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameueleza Ujumbe huo wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwamba Zanzibar bado inahitaji kuendelea kuungwa mkono na Taasisi za Umoja huo katika harakati zake za Maendeleo na Ustawi wa Jamii.

Amefahamisha kwamba mradi wa huduma za maji safi na salama katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba umepewa kipaumbele katika jitihada za kuweka miundo mbinu.

Mapema Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa aliyepo Nchini Tanzania Bw. Alberic Kacou alimueleza Balozi Seif kwamba Umoja huo kupitia Mashirika yake ya Umoja huo (UNDP) yatajitahidi kuendelea kuangalia mazingira ya kusaidia sekta ya Afya, Chakula na Lishe.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.