Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea kesho (Oktoba 13 mwaka huu) kwa timu kumi kupambana kwenye viwanja vitano tofauti katika raundi ya saba ya ligi hiyo yenye timu 14.
Polisi Morogoro itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati mwamuzi wa FIFA, Oden Mbaga atakuwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuchezesha mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons na Oljoro JKT.
Jijini Tanga, Simba itakuwa mgeni wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha.
Mechi nyingine za kesho ni Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi, na Mtibwa Sugar watacheza na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Wakati huo huo, Azam imeomba mechi zake za nyumbani dhidi ya Yanga na Simba zichezwe kwenye uwanja wake wa Azam Complex ulioko Chamazi badala ya Uwanja wa Taifa.
Nayo Ruvu Shooting imeomba mechi yake ya ugenini dhidi ya Yanga ya Oktoba 20 mwaka huu ichezwe Uwanja wa Taifa badala ya Uwanja wa Azam Complex.
Maombi hayo yatawasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Ligi ya TFF kinachotarajiwa kufanyika kesho (Oktoba 13 mwaka huu) kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
No comments:
Post a Comment