Habari za Punde

*YANGA, SHOOTING SASA KUKIPIGA TAIFA KESHO

 Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kati ya Yanga na Ruvu Shooting uliopangwa kuchezwa kesho (Oktoba 20 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi sasa umehamishiwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.
 
Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na maombi ya timu hizo mbili kutaka mechi ichezwe Uwanja wa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ambazo zimeridhiwa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwemo siku hiyo uwanja huo kutokuwa na mechi.
 
Viingilio katika mechi hiyo itakayokuwa chini ya mwamuzi Amon Paul kutoka Mara ni sh. 5,000 viti vya kijani na bluu, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP B na C na sh. 20,000 kwa VIP A.
 
Pia Kamati ya Ligi imekataa ombi la timu ya Azam kutaka mechi zake za nyumbani za ligi hiyo zichezwe dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Chamazi kutokana na sababu za kiusalama.
 
Nayo Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa kesho (Oktoba 20 mwaka huu) katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
 
Mchezo huo namba 56 wa kukamilisha raundi ya nane utachezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo atakayesaidiwa na Hamis Chang’walu na Omari Kambangwa, wote kutoka Dar es Salaam.
 
Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili (Oktoba 21 mwaka huu) kwa mechi tatu. JKT Ruvu itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi, Mgambo Shooting itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Tanzania Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.