ELECTIONS COMMITTEE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UAMUZI KUHUSU RUFANI DHIDI YA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU MKOA WA MWANZA (MZFA), MKOA WA GEITA (GEREFA) NA KUHUSU MICHAKATO YA UCHAGUZI YA VYAMA WANACHAMA WA TFF NA WANACHAMA WAO
OKTOBA 31, 2012
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 8(2), 10(6), 12(1) na 26(2) na (3) katika kikao chake kilichofanyika Oktoba 30, 2012 ilijadili rufani dhidi ya Kamati za Uchaguzi za MZFA na GEREFA na michakato ya uchaguzi ya vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Mwanza, Rukwa, Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA), Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) na Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na kutoa uamuzi kama ifuatavyo;
1. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)
(a) Rufani ya Ndg. Jackson Manji Songora: Kamati ilijadili rufani iliyowasilishwa na Ndg. Jackson Manji Songora dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kumpitisha Ndg. Jumbe O. Magati kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MZFA, kwamba Kamati ya Uchaguzi ya MZFA ilikosea:
(i)Kupokea Statement of Results ya Baraza la Mitihani Tanzania yenye jina la Fredrick J. Magati wakati jina la mgombea alilojaza kwenye fomu ya maombi ya uongozi ni Jumbe O. Magati.
(ii)Kumsaili Jumbe O. Magati kwa kuwa hakuwasilisha nakala halisi ya cheti cha elimu yake.
(iii)Kumpitisha Ndg. Jumbe O. Magati kugombea uongozi na kuwa Ndg. Jumbe O. Magati hana sifa zinazokidhi matakwa ya Katiba ya MZFA Ibara ya 29(2).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia maelezo ya Mrufani na ilijiridhisha kuwa rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Songora haikutanguliwa na pingamizi mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, hivyo ilikosa sifa ya kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1); Katiba ya MZFA Ibara ya 47 na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 26(2), Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba na kanuni za uchaguzi, ilimuhoji Ndg. Magati kuhusu elimu yake na majina yaliyo kwenye Statement of Results na fomu yake ya maombi ya uongozi.
Baada ya kupitia vielelezo na maelezo yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu majina ya Ndg. Jumbe O. Magati, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa Jumbe O. Magati na Fredrick J. Magati ni mtu huyo huyo. Kamati ya Uchaguzi imetupa rufani ya Ndg. Patrick Manji Songora.
2. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA)
(a) Rufani ya Ndg. Abdallah H. Hussein: Kamati ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Abdallah H. Hussein ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Geita. Kamati ilipitia vielelezo vilivyowasilishwa mbele yake na Mrufani na ilijiridhisha kuwa vielelezo hivyo vinakidhi kuthibitisha kuwa mwombaji uongozi ni Mkazi wa Mkoa wa Geita. Kamati inakubaliana na maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg. Abdallah H. Hussein kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
(b) Rufani ya Ndg. Aziz Mwamcholi: Kamati ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Aziz Mwamcholi ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa GEREFA, kwa kigezo cha kushindwa kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari. Kamati ilipitia maelezo ya Ndg. Mwamcholi na ya Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA na ikajiridhisha kuwa Ndg. Mwamcholi hakukidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, hususan Ibara ya 10(5). Kamati imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA wa kutompitisha Ndg. Mwamcholi kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa GEREFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetupa rufani hiyo.
(c) Rufani ya Ndg. Kaliro Samson: Ndg. Samson aliwasilisha rufani kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kigezo cha kutowasilisha cheti cha kuhitimu elimu ya kidato cha nne. Kamati ilipitia maelezo na vielelezo vya rufani ya Ndg. Samson nay a Mrufaniwa na kujiridhisha kuwa nakala ya cheti cha elimu ya kidato cha sita inakidhi matakwa ya Katiba ya GEREFA Ibara ya 29(2). Kamati inakubaliana na maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg. Kaliro Samson kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
3. Mchakato wa Uchaguzi Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili mchakato wa uchaguzi wa MZFA ikiwa ni pamoja na mchakato wa uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ukerewe (UDFA), baada ya uchaguzi wa awali wa UDFA kuwa umefutwa na Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kutokana na Kamati ya Uchaguzi ya UDFA kutozingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Baada ya maelezo ya kina ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa UDFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu za uchaguzi uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya UDFA kwa kutozingatia kikamilifu maagizo ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na hivyo kusababisha mkanganyiko katika mchakato wa Uchaguzi ambao kwa wakati mmoja ulikuwa na Kamati mbili za Uchaguzi kusimamia uchaguzi huo. Mikanganyiko inayojionyesha dhahiri na kusababisha nafasi zote sita zinazogombewa katika mchakato unaoendelea kuwa na mgombea mmoja mmoja tu katika kila nafasi, imeufanya mchakato wa uchaguzi wa UDFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka yake ya kikatiba Ibara ya 49(1) ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 10(6) na 26(2) na (3) imeamua:
(i)Kuzifuta Kamati zote za Uchaguzi za UDFA zilizoteuliwa na Kamati ya Utendaji ya UDFA kabla ya baada ya mchakato wa uchaguzi wa sasa wa UDFA.
(ii) Kuufuta Uchaguzi wa UDFA uliokuwa ufanyike Novemba 5, 2012. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya kwa tarehe zitakazopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya MZFA baada ya kupata maelekezo ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
(iii) Kuiagiza Kamati ya Uchaguzi ya MZFA katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Ibara ya 6 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF kutoiruhusu UDFA kushiriki Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa MZFA kwa kuwa UDFA imeshindwa kuzingatia matakwa ya Katiba kuhusu ukomo wa mamlaka ya Kamati ya Utendaji na kufanya uchaguzi kwa wakati muafaka unaozingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
4. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA)
Kwa kuzingatia changamoto za kuijenga TWFA ambayo bado ni change, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekubali ombi la TWFA la kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi kwa wiki mbili. Uchaguzi wa TWFA ngazi ya Taifa sasa utafanyika Novemba 18, 2012.
5. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)
Uchaguzi wa viongozi wa FRAT utafanyika Novemba 17, 2012 kama ulivyopangwa.
6. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)
TFF imesimamisha kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa RUREFA kutokana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya RUREFA kuendeleza malumbano kati yao kuhusu uhalali wa uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA, uteuzi ambao ulifanywa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA, Oktoba 18, 2012. Kwa kuwa hali hii imetokea tena baada ya Kamati ya Utendaji ya RUREFA kuwa imepewa fursa ya kikatiba kuteua Kamati ya Uchaguzi na ni mwendelezo wa mgawanyiko ndani ya Kamati ya Utendaji ya RUREFA unaoathiri mchakato wa uchaguzi wa chama hicho, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatafakari hatua muafaka za kikatiba na kikanuni zitakazoondoa ukwamishaji wa mchakato wa Uchaguzi wa RUREFA unaosababishwa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA. Uamuzi kuhusu mustakabali wa Uchaguzi wa RUREFA utatolewa baada ya kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Novemba 6, 2012.
7. Mchakato wa Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na Chama cha Makocha (TAFCA)
Uamuzi kuhusu mustakabali wa uchaguzi wa SPUTANZA na TAFCA utatolewa baada ya vyama hivyo kuwasilisha taarifa za kina kuhusu michakato ya chaguzi za wanachama wao katika ngazi ya mikoa, katika kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Novemba 6, 2012.
Moses Kaluwa
Mjumbe- Kamati ya Uchaguzi TFF
No comments:
Post a Comment