Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wapya wa Chama cha Netiboli Mkoa wa Dar es Salaam (CHANEDA), wanatarajiwa kutambulishwa Ijumaa katika tukio litakalohusisha mechi kadhaa za netiboli baina ya timu zilizopo mkoani humo.
Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa CHANEDA, Michael Maurus, utambulisho huo utaanza saa nane mchana kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Alizitaja timu zitakazopambana katika utambulisho huo kuwa ni Kaza Roho ya Kiwalani na Majumba Sita ya Ukonga (wanaume), huku pia zikiwamo timu za watoto ambazo ni Kiwalani Kids na Ukonga Kids.
“Kwa upande wa timu za wanawake, zilizothibitisha kushiriki ni Uhamiaji, Bandari Queens A, Bandari Queens B, CBE na Chuo Kikuu cha Tumaini,” alisema Maurus.
Aliwataja viongozi watakaotambulishwa siku hiyo baada ya uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita kuwa ni
Winfrida Emmanuel (Mwenyekiti), Pili Mogella (Makamu Mwenyekiti), Joseph Ng’anza (Katibu Mkuu), Christina Kimamla (Katibu Msaidizi), Anitha Lunogela (Mhazini) na Maurus.
Maurus aliwataja wajumbe kuwa ni Khadija Ally, Zainab Seif, Georgina Kasembe na
Mussa Sambala ambapo aliwataka wadau wa netiboli na michezo kwa ujumla jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi siku hiyo kuwafahamu viongozi wao, lakini pia kushuhudia mechi hizo.
No comments:
Post a Comment