Habari za Punde

*YANGA YAENDELEA KUJICHIMBIA KILELENI YAICHAPA COAST UNION 2-0


TIMU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, leo imeendelea kujiimarisha na kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuwagalagaza Wagosi wa Kaya, Coast Union kwa kipigo cha mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga jioni ya leo.

Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi hiyo, ikiwa katika nafasi nzuri baada ya kuanza ligi hiyo kwa kusua sua na kupoteza michezo yake kadhaa, huku watani wao wa Jadi wakifanya vizuri, ambapo kwa sasa kibao hicho kimegeuka.

Kwa ushindi huo sasa Yanga imefikisha jumla ya Pointi 29, huku ikiwa kileleni mwa ligi hiyo, ikifuatiwa na Azam Fc yenye Pointi 24, huku watani wao Simba wakiwa katika nafasi ya tatu, ikiwa na Pointi 23.

Mabao ya Yanga yalifungwana Didier Kavumbagu dakika ya 28, kufuatia pasi ya mwisho ya Simon Msuva, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.  

Kipindi cha pili, Yanga walirejea na moto wao tena na iliwachukua dakika 17 tu kuandika bao la pili, mfungaji Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliyeuwahi mpira ambao aliuokosa beki wa Coastal, Mbwana Hamisi na kuutumbukiza nyavuni kiulaini.

Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Nurdin Bakari, Frank Domayo, Simon Msuva, Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbangu/Said Bahanuzi.
Coastal Union; Juma Mpongo, Ismail Amour Khamis, Juma Jabu, Jamal Macherenga/Othman Omar Tamim, Mbwana Hamisi, Jerry Santo, Soud Mohamed, Razack Khalfan, Daniel Lyanga, Atupele Green/Lameck Dayton na Suleiman Kassim ‘Selembe’.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.