Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, akifunua kitambaa kuashiria kuzindua rasmi Skuli Mpya ya Sekondari ya Mikindani Dole Wilaya ya Magharibi, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, akimpongeza Mwakilishi wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Uchumi na Elimu, Nobuyuki Tanaka, ambaye Taasisi yake imegharamia ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Mikindani Dole.
Bibi Tiba Vuai, akionekana mwenye furaha akipokea ufunguo wa chumba chake kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, katika hafla ya uzinduzi wa jengo lao lililofanyiwa matengenezo makubwa.
*********************
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe haitakuwa na mjadala katika jukumu lake la kuendelea kuwatunza wazee wasiojiweza wanaosihi katika makazi yao waliyotayarishiwa mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua majengo yaliyofanyia matengenezo makubwa pamoja na miundo mbinu katika makaazi ya wazee yaliyopo Sebleni Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mchango wa wazee ni kubwa katika Taifa hili hasa wakati wa harakati za kupigania ukombozi wa Visiwa hivi jambo ambalo halina budi kutekelezwa na kuenziwa.
Alisema suala la ujenzi wa makaazi ya wazee wasiojiweza ni moja kati ya ahadi zilizotolewa na Chana cha Afro Shirazy Party mara baada ya Mapinduzi na serikali ya Mapainduzi ya Zanzibar inaandaa sera Maalum ya kuweka taratibu ya kuwatunza wazee kisheria .
“ Utaratibu wa kuendelea kuwatunza wazee upo kama kawaida kwani tunaelewa kwamba Jamii isiyo na utaratibu huo inaeleweka kwamba imepotoka kabisa”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa mashirika ya Kitaifa na Kimataifa zikiwemo Taasisi Binafsi kushirikiana na Serikali katika kuwatunza wazee na kutoa rai kwa wanafunzi wa vyuo Vikuu na Sekondari kutenga siku maalum ya kujumuika na wazee katika harakati zao za usafi wa mazingira.
Naye Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohd alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwaondoshea aibu iliyokuwa ikiwapata wazee wanaonyanyasika kutokana na ukosefu wa makaazi.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Fatma Gharib Bilal alisema ujenzi wa majengo hayo yaliyojumuisha nyumba moja, ukumbi wa Mikutano, sambamba na miundo mbinu ya umeme na maji umegharimu zaidi ya Shilingi MKilioni 429,900,000/-
Matengenezo hayo yamekuja kufuatia kuungua kwa moto nyumba hiyo ya wazee usiku wa terehe 6/1/2011 ,ukosefu wa uzio uliosabisha wizi wa vitu vyao na ubovu wa miundo mbinu ya maji na umeme.
Katika mwishoni mwa maendeleo ya shamra shamra za kutimia miaka 49 ya mapinduzi ya Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliifungua rasmi Skuli mpya ya Sekondari ya Mikindani iliyopo Dole Wilaya ya Magharibi.
Skuli hiyo mpya inatarajiwa kuwaunganisha wanafunzi wa Skuli za Vijiji vya Dole, Kianga, Langoni, Mwenge na Kijichi ikiwa na uwezo wa kuchukuwa Wanafunzi 320.
Zaidi ya shilingi Bilioni Moja nukta Moja zilizotolewa mkopo na Benki ya Dunia zimetumika katika ujenzi wa Skuli hiyo yenye majengo manne,Maabara, Maktaba ikiwa na wanafunzi 160 na walimu 16.
Akizungumza na Walimu wanafuni na wananachi wa maeneo hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kutafuta Walimu wenye sifa sambamba na Vifaa ili kujenga Taifa bora lenye wataalamu wa kutosha.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Taifa bado lina upungufu wa wataalamu, hivyo wanafunzi nchini wana nafasi ya kuzitumia fursa zilizopo ambazo tayari serikali imeshawajengea mazingira bora ya kielimu.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee alisema mradi wa uimarishaji wa elimu ya lazima Zanzibar chini ya Mkopo wa Benki ya Dunia umekusudia kujenga skuli 19 Zanzibar ambapo kila Wilaya itakuwa na Skuli mbili za aina hiyo.
Nd. Abdulla alisema mradi huo unaotarajwa kugharimu jumla ya dola za Kimarekani Milioni 42,000,000 sawa na Shilingi Bilioni 62 za Kitanzania unahusisha pia uchapishaji wa Vitabu.
Naye kwa upande wake Mwakilishi wa shirika la Fedha Duniani {WB } katika masuala ya Elimu na Uchumi Bwana Nobuyuki Tanaka ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua zake za kuimarisha sekta ya elimu.
Bwana Tanaka alisema hatua hiyo itaiwezesha Zanzibar kwenda sambamba na mabadiliko ya haraka ya sayansi na teknolojia ambayo tayari yanakamilika katika mfumo wa Digital.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
11/1/2013.
No comments:
Post a Comment