Na Mwandishi Wetu
MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata ameendelea kung’ara kimataifa baaada ya kushinda tuzo ya Nigeria’s Next Super model na kuwa mwanamitindo bora barani Afrika wa mwaka 2012 (Africa’s Most Outstanding Model 2012).
Tuzo hiyo hutolewa kwa wanamitindo ambao bado wanailetea sifa Afrika kimataifa na Flaviana amekuwa katika chati ya juu.
Mwaka jana Desemba, Flaviana alishinda tuzo nyingine ya uwanamintindo bora kutoka kwa diaspora ya Waafrika.
Flaviana kwa ambaye kwa sasa anaishi na kufanya kazi ya uanamitindo New York nchini Marekani kupitia shirika la Wilhelmina Models, mpaka sasa ameweza kuitangaza Tanzania kimataifa kutokana na umahiri wake katika maonyesho ya mavazi.
Tangu ashinde taji la Miss Universe Tanzania mwaka 2007, Flaviana amekuwa aking’ara katika kona zote za dunia na hasa baada ya kumaliza katika nafasi ya sita katika mashindano ya kimataifa ya Miss Universe, huku Tanzania ikishiriki kwa mara ya kwanza.
Ameweza kushiriki katika maonyesho ya mavaz mengi Ulaya na Amerika huku akitoa misaada mingi kwa Watanzania wenzake ambao wamekuwa na ndoto ya kufika mbali katika fani hiyo.
Kwa sasa Flaviana anaendesha taasisi yake, Flaviana Matata Foundation ambayo inasomesha watoto wa kike 16 na mwaka jana alitoa msaada wa vifaa vya kuokoa maisha kama sehemu ya kumbukumbu ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba huku ikiwa kumbukumbu ya kifo cha mama yake mzazi katika ajali hiyo ya mwaka 1996.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Compass Communication Tanzania Limited, Maria Sarungi Tsehai alisema kuwa wamejisikia faraja sana kwa kumvumbua mwanamitindo huyo ambaye kwa sasa anashika chati ya juu Tanzania na nje ya nchi.
Maria alisema kuwa Flaviana amedhihirisha ubora wake na mpaka sasa amepitiliza kiwango cha kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake, ndoto ambayo alikuwa nayo muda mrefu.
No comments:
Post a Comment