Habari za Punde

*MAKAMANDA WA VIKOSI VYA ULINZI NA USALAMA ZANZIBAR WAPONGEZANA BAADA YA KAZI NZITO YA GWARIDE LA MAPINDUZI

 Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akiwapongeza makamanda wa vikosi vilivyoshiriki sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar mwaka huu wakati wa hafla ya kupongezana iliyoandaliwa na Makamanda wa vikosi hivyo juzi usiku katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar.
 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Suleiman Iddi, akimtunza mtanashati Maryam Juma, katika wimbo wake wa  kusifu mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 49 kwenye tafrija ya kupongezana makamanda baada ya kumaliza gwaride la shereh hizo Januari 12 mwaka huu.
 Uzalendo ulimshinda Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohd Aboud Mohd, na kuamua kujumuika na Kikundi cha Utamaduni cha Diamond Modern cha JKU kwenye tafrija ya makamanda kupongezana baada ya kumaliza kuchapa gwaride uwanja wa amani.
 Baadhi ya Makamanda wa Vikosi vya ulinzi na usalama wakitafakari sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar mwaka huu wakiwa kwenye tafrija ya kupongeza Bwawani Mjini Zanzibar.
Ilikuwa ni siku ya furaha kwa makamanda wa Vikosi vya ulinzi na usalama wakipongezana baada ya kazi nzito ya kuchapa gwaride Januari 12 mwaka huu wa 2013. Picha Zote na Hassan wa Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais, Zanzibar
**************************
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujiandaa mapema na maandalizi makubwa ya maadhimisho ya sherehe za mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 50 sawa na Nusu karne ambazo zitatarajiwa kuwa za Kihistoria.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa kauli hiyo  wakati wa tafrija maalum ya kupongezana na kuelewana kwa Maafisa wa Gwaride iliyofanyika katika Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema ili kufanikisha azma hiyo ya Serikali lazima kila Mashirika, taasisi, Jamii na hata watu binafsi wanapaswa kuanza na maandalizi mapema kwa lengo la kupata ufanisi unaokusudiwa.
Amesema Serikali itaendelea kuunga mkono Vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuwa ndivyo vinavyonafasi kubwa ya kusherehesha vyema katika kilele cha sherehe hizo za mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif alieleza kwamba Vikosi vya ulinzi na usalama vimefanya kazi mwaka huu iliyopelekea kufurahisha na kupendeza miongoni mwa wananchi walioshuhudia maadhimisho hayo.
“ Lazima niungame kwamba sherehe za mwaka huu zilikuwa za aina yake hata baadhi ya wajumbe walioshuhudia maandalizi ya mwisho ya gwaride hilo walipendekeza baadhi ya askari kutunzwa kutokana na ukakamavu waliouonyesha”. Balozi Seif aliwapongeza maafandi hao kwa kazi nzito walioifanya.
Alifahamisha kwamba Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964  yameleta faida kubwa kwa wananchi waliowengi na kuwafanya kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya kusherehekea sherehe hizo.
Akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya sherehe na maadhimisho ya Taifa Balozi Seif, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohd Aboud Mohd alisema majeshi ya ulinzi yameonyesha umahiri mkubwa katika kuchapa gwaride.
Mh. Aboud Alieleza kwamba Serikali inajivunia kazi kubwa inayotekelezwa na majeshi ya ulinzi na usalama Nchini hasa wakati jamii inapokumbwa na majanga na kupelekea maafa.
Mapema Kamanda wa Brigedi 101 Zanzibar ambae ndie mkuu wa Gwaride hilo Bridedia General Sharif Sheikh ameahidi kwamba Vikosi vya ulinzi na usalama vitaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuona maandalizi ya maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 50 yanafanikiwa vyema.
Brigedia General Sharif Sheikh alieleza matumaini yake kwamba sherehe zijazo zitakuwa za aina yake zinazotarajiwa kuwa za kistoria ndani ya Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla.
Tafrija ya Makamanda na maafisa hao wa Vikosi vya ulinzi na usalama imekuja baada ya kazi kubwa na ngumu iliyofanywa ba Vikosi vyua ulinzi na usalama katika kufanikisha gwaride la maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi zilizochukuwa takriban siku 30.
Burdani safi iliyokuwa ikitolewa na Kikundi cha Diamond Modern Taarab kutoka Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar { JKU } ilianikiza ndani ya ukumbi huo wa Bwawani hasa pale ulipoimbwa wimbo wa mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 50 chini ya mwimbaji Mtanashati Maryam Juma.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/1/2013.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.