Habari za Punde

*MAMA SALMA ATEMBELEA AMREF NA POUR FOUNDATION NCHINI UFARANSA

 Rais wa AMREF France Bwana Nicolas Merindol akimkaribisha Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Mama Salma Kikwete kwenye makao makuu ya shirika hilo jijini Paris nchini Ufaransa, jana na baadaye viongozi hao walifanya mazungumzo juu ya ushirikiano zaidi wa taasisi hizo katika masuala ya afya na elimu. PICHA NA JOHN LUKUWI 
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Mwanzilishi na Rais wa Foundation Pour  l¨ Enfrance Mama Anne Aymone Giscard d' Estaing na Mke wa Rais Mstaafu wa Ufaransa Bwana Valery Giscard d' Estaing, wakati Mama Salma alipotembelea makao makuu ya taasisi hiyo jijini Paris Ufaransa jana. Mama Salma yupo nchini Ufaransa akifuatana na Rais Kikwete kwenye ziara ya kiserikali nchini humo:
*****************************

*Wadau wa maendeleo waiwezesha WAMA kuwasaidia wanawake na watoto


Na Anna Nkinda - Paris
Ushirikiano wa pamoja baina ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na wadau wa maendeleo nchini umeiwezesha taasisi hiyo kuwasaidia na kuwainua wanawake kiuchumi ambao wameweza  kujishughulisha na kazi za ujasiriamali na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Pia Taasisi hiyo imeweza kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi jambo ambalo limewafanya watoto hao wapate elimu  sawa watoto wengine wenye wazazi  na kuimarisha afya za mama wajawazito na watoto
Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati alipotembelea Taasisi inayoshughulika na masuala ya watoto (France Parrainages)  kiliyopo mjini Paris ambacho kinafanya kazi na Kituo cha Ufaransa cha  kuwaangalia watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Partage Tanzania inayohudumia watoto yatima katika mkoa wa Kagera.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa  WAMA alisema kuwa Taasisi hiyo imeweza kujenga shule ya Sekondari ya WAMA – NAKAYAMA iliyopo Rufiji Mkoani Pwani ambayo ina wanafunzi  247 ambao ni watoto yatima  na matarajio ya baadaye ni kuwa na wanafunzi 780.
“Katika mkoa wa Lindi tumejenga mabweni ya wanafunzi wa sekondari wa kike,  tunagharamia masomo ya Sekondari kwa  wanafunzi 250 na wanafunzi 16 wa elimu ya juu kutoka mikoa yote nchini”, alisema Mama Kikwete.
Aliendelea kusema kuwa Taasisi hiyo  imeweza kuwasaidia wanawake kiuchumi  na kuwafanya waweze kuongeza kipato cha familia zao, kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vidogo vidogo ambavyo vinaweza kutengeneza bidhaa za kusindika za vyakula na kuziuza.
Kwa upande wake Charline Flauge’re ambaye ni msimamizi wa Programu za Kituo cha Ufaransa cha  kuwaangalia watoto upande wa Afrika alisema kuwa Taasisi ya Partage Tanzania ambayo inahudumiwa na kituo hicho inafanya kazi nchini katika mkoa wa Kagera ambayo ni moja ya nchi tatu muhimu  kutokana na idadi ya watoto wanaowahudumia kufikia 10000.
Alisema kuwa watoto hao yatima wanaishi vijijini na familia zao zinajishughulisha na kazi za ukulima mdogo wa kahawa na migomba wao wanatoa ufadhili ambao unawasaidia waweze kuishi na familia zao na kupata upendo wa ndugu bila ya kuishi katika vituo vya kulelea watoto yatima
Flauge’re alisema, “Tunashukuru kwa kuwahudumia watoto hawa ambao wameweza kukua wenyewe ndani ya familia zao za mama,  kaka au dada, ufadhili huu umeweza kumsaidia mzazi aliyebaki hai, bibi na babu zao kuwaangalia na hivyo  kukua katika afya njema  na mazingira yao waliyozaliwa
Alimalizia kwa kusema kuwa ufadhili huo hautoi fedha na vitu  peke yake bali pia unajenga mahusiano baina ya watoto na wafadhili wao ambao wanaishi nchini Ufaransa kwani watoto wanawaandikia wafadhili barua na kuwasiliana nao na wakati mwingine wanakuja kuwasalimiana nchini Tanzania na hivyo kujifunza mila na desturi za pande zote mbili.
Taasisi  ya WAMA ilianzishwa  mwaka 2006 ikiwa na malengo ya kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike ambao hawakupata nafasi ya kusoma, kuimarisha afya ya mama wajawazito na watoto, kuwainua wanawake kiuchumi na kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.