Habari za Punde

*SHIRIKA LA NDEGE LA PRECISION AIR YAZINDUA SAFARI ZAKE ZA MKOANI MBEYA

 Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri wa Wizara ya Uchukuzi, Peter Lupatu, akikata utepe kuzindua Safari za Ndege za Shirika la Precision Air za Mbeya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Precision Air, Michael Shirima. 
  Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri kutoka Wizara ya Uchukuzi, Peter Lupatu, akishuka kutoka katika ndege ya shirika la Precision Air wakati wa uzinduzi wa Safari za Mbeya – Dar kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe kabla ya kukata utepe kuzindua safari hizo. Nyuma yake ni Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Michael Shirima. 
 Mwenyekiti wa Bodi ya Precision Air (PW), Michael Shirima, (Kushoto) akiteta jambo na abiria wa kwanza kununua tiketi ya safari ya Mbeya wakati wa uzinduzi wa Precision Air wa  njia ya Mbeya – Dar, Bw. Alfred Mwambeleko Jumatano hii.  

 Mzee akisaidiwa kupanda ndege, ambaye ni mkazi wa mkoani Mbeya wakati wa uzinduzi wa Safari za Ndege za Shirika la Precision Air za Mbeya – Dar uliofanyika Jumatano hii kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe uliofanyiwa marekebisho kutumika kwa safari za kimataifa.
*********************************
SHIRIKA la ndege la Precision Air (PW) jana lilizindua safari zake za mkoani Mbeya, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ambao umekamilika kukarabatiwa hivi karibuni na kuuwezesha utumike katika safari za kimataifa.

Huu ni ujio mpya wa safari za shirika hilo ambapo walikuwa wanaruka kuenda mkoani Mbeya kati ya miaka ya 1997 hadi 2000 wakitua kastika uwanja mdogo uliopo katikati wa mji wa Mbeya.

Uzinduzi ambao ulifanywa na Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi, Peter Lupatu kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri wa anga ulifanyika katika uwanja wa ndege wa Songwe, ambapo wakazi wa Mbeya walielezea furaha yao juu ya uzinduzi huo.

Shirika hilo lilitumia ndege yake aina ya ATR-72 yenye uwezo wa kubeba abiria 70, katika kuzindua njia hiyo mpya, kwa kuanza na ratiba ya kuruka Mbeya mara nne katika wiki (Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili) kwa nauli ya shilingi 249,000/= kwa tiketi ya kwenda na kurudi na shilingi 165,000 /= kwa tiketi ya njia moja, zikijumuisha kodi na gharama nyinginezo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Lupatu alisema kuwa hatua iliyochukuliwa na Precision Air itauwezesha mkoa wa Mbeya na majirani zake kuwa na fursa nyingi za kibiashara na maendeleo kwa upatikanaji wa usafiri wa anga katika eneo hilo.

"Natoa wito kwa wakazi wa Mbeya na majirani zake kutumia fursa hii kikamilifu iliyotolewa na Precision Air baada ya kuanzisha safari zake za kibiashara katika mkoa huu. Hii ni hatua kubwa kwa mkoa na sekta ya usafiri wa anga nchini.

"Uwepo wa usafiri wa uhakika wa ndege tunaouanzisha leo hii unaonyesha kwamba Mbeya na mikoa ya jirani sasa itapata fursa kubwa za kibiashara pamoja na kuunganishwa na miji mikubwa ya kibiashara na miji mingine duniani.

"Kuanzishwa kwa njia hii mpya itakuwa ni chachu ya ukuaji mkubwa wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huu ambazo ni pamoja na kilimo cha mbogamboga na maua, kwa kuwa sasa wakulima wanauhakika wakusafirisha mazao yao kwa wakati katika masoko yanayostahili," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Precision Air, Michael Shirima, aliiomba serikali kutafuta mwekezaji ambaye atawekeza katika uuzaji wa mafuta ya ndege katika uwanja wa ndege wa Songwe ili kuwasaidia wawekezaji katika sekta ya usafiri wa anga kupunguza gharama za uendeshaji.

"Ombi langu kwa serikali ni kuhakikisha kuwa kunakuwepo na upatikanaji wa mafuta  ya ndege ya kutosha katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa mashirika ya ndege. Kwa sasa, tunalazimika kubeba mafuta ya akiba ambayo huongeza mzigo katika ndege, hivyo inatulazimu kubeba abiria wachache na kuacha nafasi kwa ajili ya mafuta ya akiba, "alisema Bw Shirima.

Muasisi huyo wa PW pia aliiomba serikali kuhakikisha kuwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe unakuwa na vifaa bora vya kuongozea ndege kutokana na eneo lilikojengwa ili kulinda usalama wa ndege na abiria wake. Pia aliiasa serikali kufunga rada katika uwanja huo wa ndege, kama ilivyo katika viwanja vingine vya kimataifa.

Aliwahakikishia wakazi wa Mbeya kwamba shirika katika siku za usoni litaongeza idadi ya safari zake za Sogwe endapo abiria wa kwenda na marudio itaongezeka.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Norman Sigala akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni alisema kuwa anafuraha na uamuzi wa Precision Air wa kufika mkoani Mbeya kwa kuwa jitihada hizo zitapunguza changamoto za usafiri kwa wakazi wa mkoa huo za usafiri hususani usafiri wa Dar es Salaam na kuungana na miji mingine duniani.

"Uzinduzi tunaoushuhudia leo ni wa baraka kubwa kwa Mkoa wa Mbeya na majirani zake. Napenda kuwahakikishia wakazi wa Mbeya kuwa Mbeya ya leo haifanani na Mbeya ya jana na ya siku zijazo. Kwa kuwa Precision Air imezindua safari zake kwa mkoa huu, utaona mashirika mengi ya ndege yakileta ndege zao hapa. Uwepo kwa usafiri wa anga sasa kutafanya ndoto zetu za kuendeleza kilimo cha mbogamboga na matunda katika mkoa wetu kufanikiwa. Shughuli zaidi za kiuchumi sasa zitafanyika katika mkoa na hivyo kuwainua watu wetu kiuchumi," alisema. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.