TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) natarajia kucheza mchezo wa kirafiki na Cameroon katika moja ya mechi za kirafiki za Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- 'FIFA Date' zitakazofanyika duniani kote Februari 6 mwaka huu.
Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni.
Kikosi cha Cameroon kinachoundwa na wachezaji wengi wa kulipwa wanaocheza katika nchi mbalimbali duniani kitaanza kuwasili nchini Februari 3 mwaka huu.
Nchi kadhaa ziliomba kucheza na Taifa Stars katika tarehe hiyo ya FIFA, lakini Kocha wa Stars, Kim Poulsen ameamua kucheza mechi hiyo dhidi ya Cameroon ambayo nahodha wake ni mchezaji nyota wa kimataifa, Samuel Etoo Fils.
Congo Brazzaville, Equatorial Guinea, Rwanda na Swaziland nazo zilikuwa ni miongoni mwa timu zilizoomba kucheza dhidi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager.
Ukiondoa Swaziland iliyotaka mechi hiyo ichezwe Dar es Salaam, nyingine zilitaka kucheza nyumbani kwao.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakutana na Waandishi wa Habari kuzungumzia maandalizi ya mechi hiyo ikiwemo kutaja kikosi ambacho atakitumia katika mchezo huu, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kujiandaa na mechi hiyo.
Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
No comments:
Post a Comment