Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja wachezaji
22 watakaoingia kambini Januari 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
mechi za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya
Morocco itakayochezwa Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kocha Kim, wachezaji hao wanatakiwa
kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma saa 11.30 jioni tayari kwa mazoezi
yatakayoanza Januari 7 mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba
ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ally wote kutoka
Azam. Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam),
Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na
Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga),
Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto
(Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP
Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon
Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC).
Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa
na Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold
Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu
wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
CAF YAMTUMA LIUNDA KUKAGUA VIWANJA
ETHIOPIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua
ofisa wake Leslie Liunda wa Tanzania kwenda Ethiopia kukagua viwanja na hoteli
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa utoaji leseni kwa klabu
zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho
hilo.
Ofisa huyo atawasili nchini Ethiopia kesho (Januari 2
mwaka huu) ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 6 mwakani na baadaye
kupeleka ripoti yake CAF.
Utekelezaji wa kazi yake hiyo nchini Ethiopia utahusisha
wadau mbalimbali ikiwemo Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ethiopia (EFF), Wizara
ya Michezo ya nchi hiyo, viongozi wa klabu na mameneja wa viwanja husika.
No comments:
Post a Comment