Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akimkabidhi sehemu ya Magodoro Matano Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma, kwa ajili ya Hospitali ya Jimbo hilo iliyopo Mikunguni Mjini Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi mifuko 20 ya Saruji Mwakilishi wa Jimbo la Kwmtipura Mh. Hamza Hassan Juma kwa ajili ya uendelezaji ujenzi wa Matawi ya Chama hicho yaliyomo ndani ya Jimbo hilo.
Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh.Hamza Hassan Juma akipokea msaada wa Vitanda 12 kwa ajili ya Hospitali ya Jimbo la Kamtipura ili kuongezewa nguvu ya utoaji huduma Hospitali hiyo.Picha na Hassan Issa wa – OMPR - ZNZ
**********************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi msaada wa Vitanda 14 na Magodoro Matano kwa ajili ya Hospitali ya Kwamtipura ili kuiongezea nguvu ya ziada katika kutoa huduma za Afya kwa Wananachi.
Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi pia akakabidhi Mifuko 20 ya Saruji kwa uendelezaji wa ujenzi wa Matawi ya Chama cha Mapinduzi ndani ya Jimbo la Kwamtipura.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikabidhi msaada huo hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar hafla ambayo pia ilishuhudiwa na Baadhi ya Viongozi na wanachama wa chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Kwamtipura.
Akikabidhi msaada huo kwa Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma Balozi Seif alielezea kutiwa moyo na Juhudi za Uongozi na Wananchi wa Jimbo hilo za kujiletea Maendeleo sambamba na kuimarisha Ustawi wa Jamii.
Alisema Hospitali ya Kwamtipura inastahiki kupewa msukumo wa kupatiwa vifaa kutokana na mazingira ya ukubwa na ubora wake unaoendelea kusaidia wananchi sio wa Jimbo hilo bali hata wa majimbo mengine Jirani.
“ Kwenye ziara yangu ya kutembelea Taasisi za Wizara ya Afya mwaka uliopita nikiwa Hospitali ya Kwamtipura niliushauri Uongozi wa Wizara hiyo kuangalia utaratibu wa Kuitumia Hospitali hiyo kama Tawi la Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja. Na kwa Taarifa za karibuni suala hilo limekuwa likifanyiwa kazi na Uongozi huo” Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia uhai wa Chama cha Mapinduzi Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliutaka uongozi wa Jimbo hilo kuhakikisha kwamba chama hicho kinaendelea kupewa nguvu kwa lengo la kukiwezesha kufanya vyema katika utekelezaji wa ilani yake iliyonadiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu na kupata ridhaa ya Wananachi walio wengi Nchini.
Akipokea msaada huo Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi zake anazoendelea kuchukuwa za kuunga mkono nguvu za Wananachi katika miradi tofauti ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.
Mh. Hamza alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Uongozi wa Jimbo hilo utahakikisha kwamba Jimbo hilo linatarajiwa kukabidhiwa tena kwa Chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi Jimbo la Kwamtipura Bibi Stumai Mohd Mshimbe alisema msaada wa Balozi Seif utaongeza ari na nguvu kazi kwa Wanachama hao katika kujisogeza zaidi kwenye maendeleo ya chama chao.
Msaada huo wa Vitanda 12, Magororo Matano pamoja na Saruji Mifuko 20 umegharimu jumla ya Shilingi MilioniTatu na Laki Tisa { 3,900,000- }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/2/2013.
No comments:
Post a Comment