Habari za Punde

*MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL ASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA UTOKOMEZAJI WA UGONJWA WA FISTULA, JIJINI DAR

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baba wa mtoto, Elizabeth Nora kutoka Dodoma aliyelazwa katika Hospitali ya CCBRT, wakati Makamu alipofika hospitalini hapo leo Mei 23, 2013 kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utokomezaji wa Ugonjwa wa Fistula.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Dokta wa Hospitali ya CCBRT, wakati alipokuwa akitembelea katika wodi za wagonjwa waliolazwa katika Hospitali hiyo, alipofika hospitalini hapo leo, kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utokomezaji wa Ugonjwa wa Fistula. Kulia ni Mtoto Boniface Patrick akiwa na Baba yake, Patrick Luwao, Wakazi wa Dodoma, akiwa amelazwa baada ya kufanyiwa upasuaji na kuongezewa sehemu ya mguu uliokuwa mfupi.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Stellah Nzyemba, ambaye awali alikuwa mgonjwa na baada ya kutibiwa katika Hospitali hiyo ya CCBRT na kupona ameajiriwa ili kuwasaidia wagonjwa wa Fistula. Makamu alifika hospitalini hapo leo kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utokomezaji wa Ugonjwa wa Fistula.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitembelea katika Wodi ya wagonjwa wa Fistula, wakati Makamu alipofika hospitalini hapo leo kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utokomezaji wa Ugonjwa wa Fistula.
 Makamu wa Rais Dkt Bilal, akimjulia hali mtoto mgonjwa aliyelazwa katika Hospitali hiyo ya CCBRT
 Baadhi ya wasichana waliokuwa wakiugua ugonjwa huo na kutibiwa katika Hospitali ya CCBRT, ambao kwa sasa wanapewa mafunzo ya kufanya kazi za mikono.
 Makamu wa Rais Dkt. Bilal, akiwasili katika eneo lililoandaliwa maalum kwa ajili ya kufanyia shughuli za maadhimisho hayo.

 Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose, akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.
 Balozi wa Ugonjwa wa Fistula, Msanii wa Muziki wa Kizazi kipya, Mwana FA, akisoma hotuba yake kuhusiana na kuzunguka katika baadhi ya mikoa na kutoa ujumbe kwa wananchi na hasa kina mama kuhusu Ugonjwa huo.

*Salaam za Hamis Mwinjuma - Mwana FA Balozi wa Chapa Vodacom wakati wa maadhimisho ya siku ya fistula Mei 23, jijini Dar es salaam.
Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt Mohammed Gharib Bialal
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Hussein Mwinyi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Meck Said
Waheshimiwa Mabalozi
Watendaji wakuu wa Vodacom na CCBRT
Itifaki imezingatiwa
 Mheshimiwa Makamu wa Rais
Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kutujaalia afya njema na uzima kumaliza salama safari yetu hii na kutuwezesha kuwepo katika tukio hili la kuadhimisha siku ya fistula duniani.
Aidha, nawashukuru sana Vodacom kwa kuamua kuniteua kuwa balozi wa Chapa yao. Ni kutokana na ubalozi huo leo Mwana FA najikuta nikipata fursa ya tofauti ya kuwa karibu na Watanzania wenzangu na kutoa mchango wangu kwao kwa namna tofauti na ile iliyozoeleka. Hii ni heshima kubwa sana ambayo naamni ni ndoto ya kila msanii.
Mheshimwa Makamu wa Rais
Msafara ulioupokea ulianza safari yake Mei 17, 2013 Bukoba, Mkoani Kagera. Msafara huu ulianza safari yake na kupita Chato, Geita, Singida, Dodoma, Morogoro na Rufiji Mkoa wa Pwani. Kote huko msafara huu ulikuwa na jukumu moja kubwa la kuelimisha jamii kuhusu fistula na kuieleza jamii kwamba tatizo hilo linatibika na tena matibabu yake yanapatikana bila ya malipo katika Hospitali ya CCBRT kwa ufadhili wa Vodacom Foundation na Vodafone Foundation na wadau wengine. Mpango huu ni wa mfano, ni wazi unaonesha namna makampuni haya yanavyojali maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Makamu wa Rais
Maeneo yote tuliyopita, tuliifanya kazi hiyo kwa umakini na udhati mkubwa ili kuhakikisha lengo la safari linafikiwa.
Msafara niliouongoza uliwajumuisha watu takribani 25 wakiwemo wataalamu kutoka CCBRT, mwakilishi wa Vodacom, wanawake waliowahi kupatwa na tatizo la fistula na kupatiwa matibabu chini ya kampeni hii inayofadhiliwa na Vodacom na Vodafone ya nchini Uingereza, waandishi wa habari, madereva na waratibu kutoka kampuni ya Prime Time Promotion.


 Mheshimiwa Makamu wa Rais
Kazi ya kueneza ujumbe haikuwa rahisi na wala haikuwa ngumu pia. Wananchi tuliowafikia walionesha kutuelewa na kuupokea vyema ujumbe tuliowapelekea, changamoto kubwa ilikuwa ni kuhakikisha kila mmoja anakuwa tayari kuiunga mkono kampeni hii hasa akina baba. Nimetumia muda mwingi zaidi kuongea na akina baba na kuhakikisha elimu hii ya fistula inawaingia. Nimefanya hivyo nikitambua kuwa hakuna fistula bila ya baba, sisi wanaume ndio tunaowapa ujauzito wanawake, hivyo ni lazima tufahamu kuwa tunawajibu wa kumsaidia mwanamke pale inapotokea bahati mbaya anakutwa na fistula. Si vyema wala haki kuwa chanzo cha tatizo na baade tunageuka na kuwa pia chanzo cha mateso kwa wanawake kwa kuwatelekeza na kuwanyanyapaa hatua inayowaongezea mateso yakiwemo ya kisaikolojia.  

Mheshimiwa Makamu wa Rais
Nichukue nafasi hii kumpongeza Patford na Bizaire. Hawa ni waume wa Zipora na Sofia tuliokuwa nao kwenye msafara. Walitumia nafasi ya kampeni kusimulia hali ilivyokuwa katika ndoa zao baada ya wake zao kupata fistula. Nilichokipenda katika maelezo yao ni namna walivyokuwa wazi, lakini pamoja na yote walionesha uanaume wao kwa kusimama nyuma ya wake zao hadi walipopona. Hawa Mheshimiwa Makamu wa Rais ndio wanaume wa ukweli na wala sio wanaume suruali.
 Mheshimiwa Makamu wa Rais
Nilichokigundua wakati wa kampeni hii ni kwamba jamii bado inahitajia elimu zaidi kuweza kubadili mitazamo walioyonayo kuhusu fistula. Bado tatizo hili linahusishwa na imani za kishirikina na wengine wakiamini kuwa ni laana ambayo mwanamke huipata kutokana na sababu mbalimbali. Huu ni mtazamo hasi ambao jamii lazima iendelee kuelimishwa kuachana nayo, watambue kuwa Fistula ni tatizo la kiafya, na linatibika kama yalivyo magonjwa mengine, kikubwa ni kila anaepatwa na tatizo hili kujitokeza na kupata matibabu.

Kupitia wataalamu wa CCBRT na pia mashuhuda, tuliweza kuelimisha jamii kuhusu ukweli wa fistula na kwamba hakuna uhusiano wa fistula na ushirikina bali ni tatizo linalomkuta mazazi kama yalivyo matatizo mengine,na zaidi ya yote linatibika. Tuliowandolea hofu na kuwaomba kila mmoja kuwa mshirika wa kampeni hii ili kwa pamoja tuwezeshe kufikiwa kwa shabaha ya kumaliza tatizo la fistula ifikapo mwaka 2016.
Mheshimwa Makamu wa Rais
Nitumie nafasi hii kutoa rai kwa wasanii wenzangu kutumia ushawishi walionao kwenye jamii kueneza elimu ya fistula kuwa inatibika, iwapo kila msanii ataunga mkono kampeni hii na kufikisha ujumbe wa fistula kwa washabiki wake, ni dhahiri kwamba ndani ya muda mfupi sana tutakuwa na mnyororo mkubwa wa watu wenye uelewa kuhusu fistula, Ni kwa njia hiyo kazi ya kumaliza tatizo la fistula nchini itafanikiwa kwa urahisi zaidi.
Mheshimwa Makamu wa Rais.
Mwisho kabisa, niwapongeze Vodacom na Vodafone kwa jinsi wanavyojitoa kwa jamii. Napenda kuwaambia kwamba jamii inaona na kuheshimu mchango wenu, kote tulikopita wananchi hawakuona aibu kumwaga sifa kwenu. Naahidi nitatumia ubalozi  wangu kueneza kazi nzuri  mnayoifanya katika elimu, afya, uwezeshaji wanawake kiuchumi na mazingira. Najisikia fahari kubwa sana kuwa balozi wa kampuni yenye sifa nzuri na jina zuri mbele ya jamii.

Mheshimiwa Makamu wa Rais, FISTULA INATIBIKA, TUJITOKEZE KUPATA MATIBABU BILA MALIPO.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
 Wasanii 21 walioungana na kuimba wimbo wa Kidole kimoja, wakitoa burudani jukwaa.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utokomezaji wa Ugonjwa wa Fistula, yaliyofanyika leo Mei 23, 2013 Jijini Dar es Salaam.
****************************

*Zaidi ya wagonjwa 1365 wapata tiba ya Fistula
•Ni kutokana na ushirikiano wa Vodacom, CCBRT na serikali.
Tangu Kampuni ya Vodacom, Hospitali ya CCBRT na Serikali, kuzindua kampeni dhidi ya ugonjwa wa fistula, tayari mpango huo umeweza kuwanufaisha na kuwapatia tiba wanawake wapatao 1365 nchini Tanzania.

Hayo yalitanabaishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Erin Teleman, katika kilele cha wiki ya Fistula ambayo ilianza Mei 17 mwaka huu Bukoba mkoani Kagera na kupita Chato, Katoro, Geita, Singida, Dodoma, Morogoro, Rufiji na kuhitimisha  wiki ya fistula duniani jijini Dar es Salaam.
Alisema CCBRT kwa kushirikiana na Vodacom ilimteua balozi wake, Balozi wa Chapa Vodacom ambaye ni msanii wa muziki wa hip hop Hamis Mwinjuma (MwanaFA),  ili kuweza kufanikisha kueneza elimu juu ya ugonjwa wa fistula sehemu mbalimbali nchini na kuweza kufikia lengo la kuamliza fistula ifikapo mwaka 2016.

“Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wanawake 3,000 wanapata tatizo la ugonjwa wa fistula kila mwaka kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu,” alisema Erin Teleman, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT na kuongeza kuwa,
“Mikakati yetu ni kuhakikisha tunapunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha wanawake wanaougua ugonjwa wa fistula ili kurejesha hadhi na heshima ya wanawake. Hadi sasa tumefanya kazi nzuri sana lakini nina imani kuwa tunaweza kufanya zaidi ya hapa.


Tumetengeneza mtandao wetu wa mabalozi ambao wataendesha kampeni nchi nzima zitakazosaidia kupata wanawake wenye matatizo haya na kutengwa sehemu mbalimbali nchini.”

Ugonjwa wa fistula ni hali ya ulemavu inayomfanya mwanamke kushindwa kuuzuia mkoja na sambamba na kupata maumivu makali hali inayosababishwa na ufanyaji wa kazi wa muda mrefu. Kwa wastani kuna zaidi ya kesi mpya za wagonjwa wa fistula kila mwaka nchini Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu huyo alisema kuwa mgonjwa anapochelewa kupata tiba kwa wakati hupelekea kusababisha usugu wa tatizo la fistula sambamba na kupata matatizo ya kisaikolojia ambapo pia mara nyingi wanawake wamekuwa wakitengwa kijamii.

Aidha, Mtendaji huyo wa CBBRT alisema kuwa upasuaji wa kuondoa tatizo la fistula ni rahisi na wenye gharama nafuu ambapo aliongeza kuwa takwimu zinaonyesha hadi sasa kiasi cha wanawake 24,000 hawajapata huduma ya matibabu ya ugonjwa wa fistula.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Rene Meza, mpango huo umeweza kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni nane ikiwa na madhumuni kwa ajili ya kuwapatia tiba bure wanawake wenye ugonjwa wa fistula.


Aidha, Meza aliongeza kuwa kiasi hicho cha fedha ni mahususi kwa ajili ya kutoa tiba kwa wanawake wenye ugonjwa huo wa fistula nchi nzima.
Kupitia huduma ya M-Pesa, Hospitali ya CCBRT inatoa huduma ya usafiri na matibabu kwa wanawake wenye ugonjwa huo wa fistula kutoka majumbani mwao hadi hospitalini na hivyo kupata matibabu sahihi.

“Huu ni mpango wa muda mrefu wa Kampuni ya Vodacom kwa kushirikiana na wadau wengine katika kujaribu kutatua matatizo ya ugonjwa wa fistula ambao unaikabili jamii na hii ni sehemu ya mchango kwa jamii wa kampuni yetu ya kuwapatia maisha bora. Tunaungana na serikali katika kuboresha  huduma ya uzazi na kupunguza vifo vya watoto wachanga,” Meza alisema.


Kupitia huduma ya uwezeshaji wa nauli kwa wagonjwa kupitia M-Pesa, idadi ya wagonjwa wa fistula ambao wamekwishapata tiba kwenye hospitali ya CCBRT imeongezeka kutoka 168 mwaka 2009 hadi kufikia 338 mwaka 2011, ambayo ni sawa na ongezeko la kiasi cha asilimia 100 katika miaka miwili.
Kampuni ya Vodacom na Hospitali ya CCBRT wameiomba wadau mbalimbali kurejesha utu kwa wanawake wote wakitanzania waliona ugonjwa wa fistula ambao unatibika.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.