Habari za Punde

*NAIBU KATIBU MKUU WA WHVUM PROF, ELISANTE AMPA 'MENO' BONDIA MSTAAFU RASHID MATUMLA

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari , Vijana , Utamaduni na Michezo (WHVUM) Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza na Bondia Mstaafu Rashid Matumla (Snake Man) alipomtembelea leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo yao Prof Elisante alimtaka Bondia huyo kuandaa mipango na mikakati ya kuhakikisha anatafuta mrithi wake katika mchezo huo kwa kuwarithisha viajana watakaofuata nyayo zake na kufika mbali katika mchezo huo kimataifa. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ,Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiwa katika mazungumzo na Bondia Mstaafu ,Rashid Matumla leo jijini Dar es Salaam alipomtembelea ofisini kwake (wa pili kushoto) ni Mkurugenzi wa Michezo katika wizara hiyo, Leonard Thadeo (kushoto) no Ofisa Vijana katika wizara hiyo, Amina Sanga.
Picha ya pamoja - Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye miwani)  Mkurugenzi wa Michezo katika wizara hiyo  Leonard Thadeo( mwenye koti jeusi kulia), Bondia Mstaafu Rashid Matumla (mwenye fulana ya mistari)), pamoja na Afisa Vijana katika wizara , Amina Sanga(kushoto). Picha zote na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO
*************************************************
*Serikali yamtaka Matumla kurithisha kipaji chake kwa vijana

Na Concilia Niyibitanga, Wizara ya Hbari, Vijana, Utamaduni na Michezo
 Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imemtaka Bw. Rashid Matumla ambaye ni bondia mstaafu katika mchezo wa ngumi za ridhaa kurithisha kipaji chake kwa vijana wengine.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Prof Elisante Ole Gabriel wakati akiongea na Bw. Matumla alipomtembelea ofisi kwake.Prof. Gabriel amemtaka kuanzisha kikundi cha vijana ambacho ataweza kukifundisha mchezo huo ili kipaji chake kisipotee ukizingatia kuwa Tanzania ina wachezaji wachache katika mchezo huo.
“Ni vema ukarithisha ujuzi wako katika mchezo wa ngumi kwa vijana chipukizi kwa kuwafundisha na kuwashauri katika mchezo huo” Amesema Prof. Gabriel.
Amesema kuwa Serikali inatambua mchango wake katika mchezo wa ngumi hapa nchini na hivyo si vema akakaa na ujuzi wake ukizingatia kuwa yeye amestaafu katika mchezo huo.
Aidha, Prof. Gabriel ameongeza kuwa kwa kufanya hivo Matumla atawasaidia vijana chipukizi kuwa Mabondia wazuri wa baade ikiwa ni pamoja na kujiajiri badala ya kujihusisha na vitendo vibaya kama matumizi ya madawa ya kulevya n.k
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Bw. Leonard Thadeo amesema kuwa kikundi hicho kinaweza pia kikajihusisha na ujasiriamali kwa kuomba mikopo katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kuwa wanamichezo pia wanatakiwa kujishughulisha na ujasiriamali ili kujiongezea kipato.
Kwa upande wake Bw. Matumla amesema kuwa amefurahi na amefarijika sana kuongea na viongozi wa wizara inayosimamia michezo na vijana kwa kuwa wameonesha kutambua mchango alioliletea Taifa hili katika mchezo huo.Matumla amesema kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa anawarithisha mabondia chipukizi na vijana wengine kipaji chake katika mchezo huo ili wawe mabondia bora wa baadaye.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.