Mshambuliaji wa Kimataifa wa timu ya Taifa na Yanga ya Jijini dar es Salaam, akiwa kazini katika moja ya mchezo wa kimataifa.
*************************************
Mhambuliaji huyo leo anatarajia kushuka dimbani kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kukosa mechi sita.
Ngasa anatarajia kuwakabili Ruvu Shooting, katika mchezo wa Ligi hiyo utakaopigwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, iwapo atapangwa na Kocha wa timu hiyo.
Baada ya kutumikia adhabu hiyo Ngasa, amelazimika kuuza moja kati ya magari yake ya kifahari ili kuweza kukamilisha zoezi hilo la kulipa deni la Sh. milioni 45, alilokuwa akitakiwa kuilipa Klabu ya Simba kutokana na maamuzi ya Kamati ya Maadili, ili kuweza kuwa huru kuitumikia timu yake ya Yanga aipendayo kutoka rohoni.
“Mpira ni mchezo wa furaha, hela si kitu, kikubwa kuliko utu, lakini pamoja na yote hayo mimi sina bifu na Simba. Isipokuwa michezo ni furaha na mimi na wala si uadui, na pia jambo hilo kwangu ni kama changamoto tu,”alisema Ngassa.
Ngassa alifungiwa mechi sita katika mashindano na TFF baada ya kubainika alisaini mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na hayo, mshambuliaji huyo alitakiwa kurejesha fedha alizodaiwa kuchukua kusaini Mkataba wa Simba SC, Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15, ambazo amemaliza kuzilipa jana jioni na kuwa huru.
Aidha Ngasa aliwataka mashabiki wa Yanga kote nchini kutulia na kusubiri matokeo na furaha baada ya kuachiwa huru, na kuahidi kufanya makubwa ili kufidi mechi zote sita alizozikosa katika Ligi inayoendelea.
No comments:
Post a Comment