HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL,
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KATIKA MKUTANO WA TATU WA AFRIKA NA ARABIA, NCHINI KUWAIT, 20 NOVEMBA, 2013
Mfalme, Sheikh
Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, Amiri wa nchi ya Kuwait na Mwenyekiti Mwenza
wa Mkutano wa tatu wa Afrika na Arabia;
Mheshimiwa
Hailemariam Dessalegn,
Waziri Mkuu wa
Ethiopia na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa tatu wa Afrika na Arabia;
Waheshimiwa
Wafalme na Koo za Kifalme;
Waheshimiwa
Wakuu wa Nchi na Serikali;
Mheshimiwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu;
Mheshimiwa
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika;
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana:
Mwanzo kabisa, nianze kwa kutoa shukrani zangu za
dhati kwako wewe Mheshimiwa Mfalme Sheikh Sabah Al-Ahmad Sabah, Amiri wa nchi ya
Kuwait, Serikali na wananchi wa Kuwait, kwa mapokezi mazuri na maandalizi makubwa
mliyofanya ya kuandaa mkutano huu. Pili, niruhusu nitoe salamu kutoka kwa
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ambaye alipenda sana kuhudhuria mkutano huu, lakini hakuweza kufanya hivyo
kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine ya kimataifa. Mheshimiwa Rais amenituma
kuwasalimu na pia kuwaeleza kuwa anautakia mkutano huu mafanikio makubwa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
Waheshimiwa
Viongozi;
Nchi za Afrika na
Arabia zinaunganishwa na mambo kadha wa kadha yakiwemo; historia, jiografia na
utamaduni. Mahusiano yetu ya kihistoria na ukaribu wa kijiografia yametusaidia
kuwasiliana kwa karne nyingi. Mawasiliano haya na mahusiano hayo, yamekuwa
katika Nyanja za biashara, dini na tamaduni. Leo hii, theluthi mbili ya idadi
ya wakazi wenye asili ya Arabia wanaishi Afrika. Nchini Tanzania, idadi kubwa
ya wananchi wetu walio ughaibuni wanapatikana katika nchi za ukanda wa Arabia. Hakuna maeneo mengine nje ya Afrika ambapo
lugha ya Kiswahili inazungumzwa kwa ufasaha kama ilivyo kwa nchi za Oman na
Yemen. Hizi ni baadhi ya sababu zinazochangia kufanya ushirikiano baina yetu
kuwa wa lazima.
Kama ambavyo
tunaelewa, mkutano wa pili wa Afrika na Arabia uliofanyika Libya mwaka 2010
uliazimia mambo mengi ya msingi yaliyolenga kukuza na kutanua uhusiano baina ya
kanda zetu hizi mbili. Kwa leo nitazungumzia kupitishwa kwa mkakati Kazi wa
Afrika na Arabia yaani (Africa-Arab Strategic Framework and its Joint Plan of
Action wa mwaka 2011 – 2016. Mkakati huu ulibainisha maeneo manne ya
mashirikiano ambayo ni: ushirikiano wa kisiasa na uchumi, biashara na mtaji,
kilimo na chakula na mahusiano ya kijamii na kitamaduni.
Ndugu Waheshimiwa;
Ni miaka mitatu sasa
tangu tuanze kutekeleza mpango wa utekelezaji wa Pamoja kwa nchi za kanda hizi
na ripoti zilizowasilishwa katika mkutano huu leo, zinaonesha bila kuficha yale
tuliyofanikiwa kuyatekeleza. Miradi mingi ya Maendeleo iliyopitishwa haijaanza
kutekelezwa na baadhi ndiyo iko katika hatua za awali ambapo hali hii imetokana
na sababu mbalimbali. Ripoti ya pamoja ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika (AU) na ile ya Sekretarieti ya Umoja wa nchi za Kiarabu imeeleza kwa
kina sababu zilizochangia kutotekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyopangwa.
Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na; ukosefu wa fedha za uendeshaji, kutokuwepo
mkakati wa ukaguzi na kushirikisha kwa kiwango cha chini sekta binafsi.
Ukitazama changamoto hizi, nyingi ziko chini ya uwezo wetu na kupitia
ushirikiano huu tunaweza kabisa kuzikabili katika kipindi tunachoweza
kujiwekea.
Ndugu Waheshimiwa;
Wote tunafahamu kuwa
dunia inapitia changamoto mbalimbali zikiwemo: athari za mdororo wa uchumi,
upungufu wa chakula, majanga yanayotokana na hali ya hewa, kutokutangamaa kwa
baadhi ya nchi sambamba na suala la ugaidi. Changamoto hizi ni kubwa na ngumu
ambazo haziwezi kukabiliwa na taifa moja peke yake. Kutokana na hali hii,
kunahitajika mashirikiano baina ya nchi za Afrika na Arabuni katika kipindi
hiki kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Kwa kuwa na mashirikiano haya, kanda zetu
hizi zitakuwa hazizungumzii tu changamoto zilizopo, bali pia zitaweza
kukabiliana na changamoto hizo kwa kutumia fursa zilizopo na hivyo kufanikisha
matakwa ya wananchi wa kanda hizi.
Nakushukuruni
sana kwa Kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment