GWIJI wa muziki wa dansi, Muhidin Maalim Gurumo ameugua
ghafla mapema leo na kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Gurumo, Juma
Mbizo na Said Mdoe, waliokuwepo Muhimbili, wameuambia mtandao huu kuwa mwimbaji
huyo mkongwe alipatwa na tatizo la shinikizo la damu na hali ikawa mbaya kabla
ya kukimbizwa hospitalini hapo. Wamesema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri na amelazwa
katika wodi ya Mwaisela namba 1.
Wajumbe hao wamesema siku chache zilizopita, Gurumo alikuwa
kwenye afya njema na hata siku ya Jumanne alihudhuria kikao cha kamati hiyo
kilichofanyika Vijana Social Hall Kinondoni.
Aidha, wajumbe hao wamedai kuwa kwa mujibu wa mke wa Gurumo,
Bi Pili, ni kwamba hata jana mwimbaji huyo alikuwa hana tatizo lolote na
alifanya mizunguko yake bila ya mikwaruzo yoyote.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha la Gurumo, Bi
Asha Baraka amewataka wapenzi wa muziki kuwa watulivu kwa vile hali ya
mwanamuziki huyo aliyeitumikia fani kwa miaka 53, inaendelea vizuri.
Tamasha la Gurumo limepangwa kufanyika tarehe 14 mwezi ujao
katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe .
Tumuombee dua mzee wetu Gurumo.

No comments:
Post a Comment