Jana tarehe 16/07/2014 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ilifanya kikao cha
kawaida cha siku moja mjini Dar es salaam. Kikao hicho kiliongozwa na
Mwenyekiti wa CCM, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilipokea taarifa ya mazungumzo
yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa upande
wa pili.
Mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji
Francis Mutungi yana lengo la kuangalia kwa kina ni kwa nini baadhi ya wajumbe
wachache wa Bunge Maalum la Katiba walisusia na kutoka nje katika awamu ya
kwanza ya Bunge hilo, na kuangalia namna watakavyorudi ili kukamilisha mchakato
wa mabadiliko ya Katiba nchini.
Kwa ujumla Kamati Kuu ya CCM imeridhishwa na mwenendo
wa mazungumzo hayo na
kupongeza juhudi hizo zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa na Vyama
husika. Kamati Kuu inapenda kueleza imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa
matunda kwa wajumbe wachache waliosusia Bunge Maalum la Katiba, kurejea Bungeni
na kumalizia sehemu ya mchakato uliobakia. Kamati Kuu inayatakia kila la kheri
mazungumzo hayo.
Kamati Kuu pia ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM
walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais. Baada ya kutafakari kwa
kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za
kugombea, ni muhimu wakazingatia Katiba, Kanuni na taratibu za Chama
zinazosimamia masuala hayo.
Kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu
za Chama kwa suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio
ya mwenendo wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo mwezi wa nane (Agosti 2014), na
kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza
kwa Kamati Kuu kuongezwa kwa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti
ya adhabu husika.
Ni
muhimu wanachama wote wakakumbuka kuwa Chama ni pamoja na Katiba, Kanuni na
taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga, jambo ambalo
halivumiliki.
Nia ya CCM kusimamia haya ni kuhakikisha Chama kinakuwa na umoja na mshikamano
ambao ni muhimu sana, hasa tunapoelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Aidha,
Kamati Kuu imewatakia kheri na fanaka Watanzania wote wakati huu wanapomalizia
mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
17/07/2014

No comments:
Post a Comment