Habari za Punde

*ACT YAUNGURUMA MKOANI SINGIDA LEO

 CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kinaweza kuunganisha nguvu na yama vingine vya upinzani ili kukiondoa chama cha mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu ujao ambapo alisema shauku kubwa ya wananchi ni kutaka kujua msimamo wa ACT Wazalendo katika kushirikiana na vyama vingine vya siasa ili kufanikisha malengo ya kuiondoa CCM katika madaraka.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Singida na Kiongozi wa ACT wazalendo Zitto Kabwe wakati akihutubia mamia ya wananchi katika uwanja wa shule ya msingi ukombozi.

"Tumedhamiria kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kuubomoa mfumo  unaonyonya wananchi. Msimamo wetu upo wazi na tumeueleza mara kadhaa"alisema na kuongeza
KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
“ACT- Wazalendo tunaunga mkono juhudi zozote za kushirikiana kwa vyama na hili linathibitishwa na jina letu Alliance na msimamo wetu kuhusu mabadiliko ya Katiba. Kubwa tunataka ushirikiano utakaonufaisha wananchi na sio ushirikiano wa kugawana nafasi za uongozi,” alisema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT alisema chama hicho hakina tatizo na kipo tayari kushirikiana na chama chochote kilichokuwa  tayari kushirikiana nao ikiwemo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Alisema umoja huo ni lazima uwe na malengo ya kujenga uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, wenye mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wananchi wote na wenye kutokomeza umasikini.

Alikanusha chama hicho kutoa  kauli yeyote dhidi ya UKAWA kama inavyoaminishwa na baadhi ya watu, bali wameweka wazi kuwa lazima misingi ya kiitikadi na kifalsafa izingatiwe katika ushirikiano wowote

"Tupo tayari kwa umoja kwani ni moja ya misingi mikuu 10 ya chama chetu na umoja ni nguvu,” alisema Zitto.

Akizungumzia hali ya umaskini kwa mkoa wa Singida, Zitto alisema pamoja na hali ya umaskini Serikali ya CCM, imeshindwa kupunguza umasikini, nchini kwa kiasi kikubwa na kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Alisema ripoti ya maendeleo ya binadamu imeonyesha kuwa Tanzania imeshuka kufikia daraja la chini la nchi zenye kiwango kidogo zaidi cha maendeleo ya binadamu.

“Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya UNDP kuhusu Maendeleo ya Binadamu duniani ya mwaka 2014 ambayo imeiweka Tanzania katika kundi la nchi zenye maendeleo ya binadamu ya kiwango cha chini.  Lakini kinachoshitusha ni kushuka kwa nafasi saba zaidi katika Kipimo cha maendeleo ya binaadamu, (HDI), ukilinganisha na mwaka 2013.

“Ushahidi mzuri wa jambo hili ni ule unaotolewa na kipimo cha Maendeleo ya Binadamu (HDI), ambacho hupima maendeleo ya binadamu katika nchi kwa kuzingatia mkusanyiko wa vigezo vya umri wa kuishi, elimu na kipato,” alisema Zitto

Alisema katika ngazi ya mikoa, ripoti hiyo  inaonyesha tofauti kubwa ya viwango vya maendeleo ya binadamu ndani ya Tanzania.

Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Iringa, Ruvuma, Mbeya, na Tanga ndiyo mikoa yenye kiwango cha juu cha maendeleo ya binadamu.

“Singida inazalisha alizeti na sasa hivi tunajua kwamba watu wanaojali afya zao, wanapenda kula mafuta ya alizeti na ukiongelea mafuta ya alizeti, basi yale yaliyo bora yanatokana katika mkoa huu. Lakini pamoja na fursa hiyo ambayo inaweza kuitumia ili kuinua hali ya maisha ya wananchi,” alisema

Alisema Mkoa wa Singida una madini lakini jambo la kushangaza bado umekuwa mkoa wa kwanza kwa umaskini huku madini hayo yakishindwa kuwanufaisha wananchi hasa wanaozunguka vijiji vya Sambaru na Londoni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira,  alisema sasa umefika wakati ni lazima nchi iwe huru kwa kuwa na misingi imara itakayoimarisha demokrasia nchini.

“Rais aitishe Bunge maalumu ili kufanya marekebisho madogo ya Katiba kuruhusu uchaguzi huru na wa haki lakini pia Wajumbe wa Tume waombe kazi na wawe wataalamu.

Alisema ACT inashauri kuitishwa kwa Bunge Maalumu ni kutokana Bunge la sasa la 10 lina uhai wa mkutano mmoja kabla ya kuvunjwa.

“Hivyo Katibu wa Bunge atangaze nafasi za wajumbe wa Tume, kamati ya Bunge ya Katiba Sheria na Utawala itafanya mahojiano ya wazi na kupata majina 22 yatakayopelekwa bungeni,” alisema Anna
 Mkazi wa Manyoni Mjini Mzee ambaye jinalake halikupatikana mara moja akichukua kumbukumbu ya picha za video kwa kutumia simu yake ya mkononi wakati wa mkutano wa ACT-Wazalendo, uliofanyika mjini Singida leo jioni.
 Wakazi wa Mji wa Singida wakishangilia viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo wakati waa mkutano huo jijini humo leo.
Zitto Kabwe, akizungumza na wakazi wa Mji wa Singida leo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.