Mwanamuziki mahiri nchini aliyejiunga na bendi ya African Stars Twanga Pepeta, hivi karibuni baada ya kuipa kisogo bendi yake ya Extra Bongo, Ally Choki na aliyekuwa kiongozi wake wa kundi la Shoo, Super Nyamwela, wanatarajia kutambulishwa rasmi na bendi hiyo Aprili 24 katika shoo maalum itakayofanyika kwenye fukwe za Escape One Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mtandao huu, wa www.sufianimafoto.com, Ally Choki, alisema kuwa hivi sasa wanaendelea na mazoezi makali ya utambulisho huo huku katika Kambi yao maeneo ya Salasala nyumbani kwa Papa Yusufedy, ambapo tayari ameandaa jumla ya nyimbo tatu alizozitaja kwa majina kuwa ni Kichwa Chini, Usiogope Maisha na No Discation, ambapo mbili kati ya hizo zitapigwa siku hiyo ya utambulisho.
Aidha Choki alisema kuwa leo wanaingia studi za Sophia Records kwa ajili ya kuanza kurekodi wimbo wa kwanza wa Kichwa Chini, na baada ya kuamilika wiki ijayo unatarajia kuanza kusikika kwenye Vituo mbalimbali ya Redio na kishwa watarekodi Video ya wimbo huo katika studio hizo hizo za Sophia Records ili wadau na mashabiki wa bendi hiyo waweze kusikiliza kazi hiyo na kuona video yake siku ya utambulisho huo.
Choki aliwataka mashabiki wa muziki wa dansi kumuunga mkono na kujitokeza kwa wingi kushuhudia kazi aliyowaandalia mashabiki wake wa tangu enzi na enzi.
''Kiukweli mimi nimejiandaa kuwaridhisha mashabiki wangu na wadau wangu naamini hawatanitupa nawasihi wahudhurie shoo hiyo ili waweze kujionea kazi na mambo matamu niliyowaandalia, na mpya nilizotua nazo kutoka nchini Japan''. alisema Choki
Naye Kiongozi wa kundi la Shoo Super Nyamwela, alisema kuwa kwa upande wa shoo tayari wameshaanza mazoezi makali ya shoo yao mpya kabambe ya 'Hewa Hewa', aliyotua nayo kutoka nchini Japan, ambayo anaamini itakuwa ni funika bovu ambayo haijawahi kuonekana katika bendi yeyote nchini.
''Kama unavyojua mimi huwa ni kazi tu, tayari vijana wameshaiva na wanatamani siku ifike tu kwani tayari wameshainasa vilivyo shoo mpya ya Hewa Hewa, ambayo kwa kweli mashabiki watafurahi sana na watabaki na historia tu siku hiyo'', alisema Super Nyamwela
No comments:
Post a Comment