Na Magreth Kinabo- maelezo
Vyombo vya habari vimeshauriwa kutoa elimu juu ya usalama barabarani ili kuifanya jamii iweze kuepukana na ajali ya barabarani badala ya kuripoti idadi ya kujeruhi watu waliokufa na kujeruhiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -(MAELEZO), Assah Mwambene wakati akitoa mada juu ya uzoefu wa vyombo hivyo nchini Tanzania(Tanzania Media Landscape) katika masuala ya usalama barabarani kwenye semina ya siku mbili kuhusu suala hilo inayoendelea kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii uliopo jijini Dares Salaam.
“Vyombo vya habari vinapaswa kufanya utafiti wa kina pale ajali zinapotokea ili kubaini chanazo cha ajali hiyo na kutoa elimu kwa jamii badala ya kuripoti idadi ya vifo na majeruhi pekee. Ikiwa vyombo vya habari vitafanya hivyo vitabadilisha mitazamo ya watu jinsi ya kuweza kuepukana na ajali hizo ambazo na vitasaidia kupunguza idadi vifo visivyohitajika na majeruhi vinavyotokana na ajali hizo,” alisema Mwambene.
Aliongeza kwamba vyombo hivyo vitoe elimu kwa jamii juu ya ufahamu wa alama za barabarani, jinsi ya kutumia barabara hasa kwenye vivuko vya watembea kwa miguu vyenye alama ya pundamilia, kuelimisha watembelea kwa miguu juu ya sheria na kanuni za usalama barabarani na kutoa waomea aibu watu wanaosababisha ajali hizo.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema vyombo hivyo na mitandao ya jamii vina wajibu wa kutoa elimu juu ya jambo hilo na kulifanya kuwa ni agenda au janga la kitaifa kama isiposimamiwa vizuri, lakini kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari mfano kutotoa picha za watu waliopata ajali zenye kuumiza na kuleta hisia mbaya kwa ndugu na jamii.
Kwa upande wake Mratibu wa shughuli za Usalama Barabarani kutoka Wizara hiyo,Dkt. Mary Kitambi alisema lengo la semina hiyo ni kuelimisha vyombo hivyo ili viweze kutoa elimu hiyo kwa jamii.
“ Tumeanzisha mradi huu baada ya kuona ajili za barabarani zimeongezeka kwa kushirikiana na Shirika la Afya la Dunia(WHO) ili kutoa mchango wa kusaidia masuala ya usalama barabarani, ili kuweza kupunguza mzigo kwa Serikali wa kuwahudumia majeruhi na madhara ya kijamii,’’ alisemaDkt .Kitambi.
Naye Mwezeshaji kutoka WHO, Mary Kessi alisema utashi wa kisiasa unahitajika ili kuweza kuleta mabadiliko kwa jamii juu ya suala hilo.
Alisema mradi huo ni wa miaka mitano na unafadhiliwa na Bloomberg Initiative for Global Road Safety (BIGRS) nchini Tanzania.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani, Inspekta Deus Sokoni aliitaka jamii kuzingatia sheria ya usalama barabarani ili kupunguza ajali hizo.
Aliongeza kwamba asilimia 76 za ajali hizo zinatokana na sababu za kibinadamu, asilimia 16 kiufundi na asilimia 8 kimazingira.
Mwezeshaji wa semina hiyo, Callie Long kutoka Canada aliwataka waandishi hao kuwa wadadasi pale ajali zinapotokea ili waweze kubobea katika uandishi wa habari juu ya suala hilo.

No comments:
Post a Comment