Na Allen Mhina na Ally Daud-MAELEZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vya Siasa vinavyoshiriki kampeni ya uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani utakaofafanyika Oktoba 25 mwaka huu, kuheshimu na kufuata sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi ili kuepuka kufanya mikusanyiko nje ya Ratiba iliyotolewa na Tume hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. R.K. Kailima leo jijini Dar es salaam imesema kuwa hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya vyama vya siasa vilivyoanza kufanya mikusanyiko ya Kampeni ya Urais nje utaratibu wa Tume.
Taarifa hiyo Imeeleza kufanyika kwa mikusanyiko hiyo yenye sura ya kampeni kunaingiliana na ratiba za kampeni za chama kingine katika maeneo husika , hivyo kusababisha uvunjifu wa amani.
Tume imeviagiza vyama hivyo kuzingatia muda wa kufanya kampeni zao kwa kufuata muda wa kuanza na kumaliza kwa mikutano yote ya vyama vya siasa ulioainishwa kwenye Kanuni ya 39 (2) ya kanuni ya uchaguzi wa Rais na Wabunge pamoja na maadili ya uchaguzi kifungu cha 2.1(C) ambapo mikutano yote hutakiwa kuanza saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni.
Aidha, vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu vimetakiwa kuwasilisha mapendekezo ya ratiba za mikutano ya kampeni zao kwa kuzingatia kanuni ndogo ya kipengele cha 3 ya kanuni za uchaguzi ambayo inaeleza kuwa ni lazima chama husika kiwasilishe ratiba inayoonyesha tarehe, muda, Mkoa na Wilaya ambapo mkutano utafanyika.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Chama chochote cha siasa kitakachotaka kufanya mkusanyiko wa kampeni kinapaswa kuwasilisha mapendekezo yake kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ili aweze kuitisha kamati ya ratiba ya kampeni ya Urais inayojumuisha wagombea wa kiti hicho ili kukubali au kukataa mapendekezo yaliyotolewa.
Imeelezwa kuwa maadili yanayosimamia uchaguzi wa mwaka 2015 yalikubaliwa na kusainiwa na Vyama vyote vya Siasa tarehe 27 Julai 2015.
Aidha, vyama vyote vilikubali kuheshimu na kutekeleza maadili hayo na ukiukwaji wa wowote wa maadili utashughulikiwa kwa mujibu wa kipengele 5.11 cha Maadili hayo.

No comments:
Post a Comment