Na Magreth Kinabo –Maelezo,Lindi
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wananchi wa Jimbo la Lindi Mjini kuhakikisha kwamba wanapiga kura ya ndiyo kwa mgombea wa kiti cha urais,Dkt. John Magufuli , mgombea kiti cha Ubunge Hassan Kaunje na wagombea viti cha udiwani ili waweze kupata maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa jana jioni na Mama Kikwete ,ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi(NEC) wa Wilaya Lindi ,wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chama hicho ya wilaya hiyo ili iliyoambatana na uzinduzi wa Ilani ya CCM kwa lengo la kuinadi na kuwanadi wagombea hao iliyofanyika kwenye uwanja wa Fisi.
“Leo nimekuja kufanya kazi hii moja ya kuhakikisha mgombea wa kiti cha urais, anashinda akiwemo mgombea wa kiti cha ubunge na wagombea wa viti vya udiwani,” alisema Mama Kikwete huku akiinadi picha ya mgombea wa kiti cha urais na kumnadi mgombea wa kiti cha Ubunge na wagombea viti vya udiwani katika kata mbalimbali kupitia chama hicho.
Mama Kikwete aliongeza kwamba ikiwa kila mtu atatoka na kufanya kampeni ya nguvu jimbo hilo litapata kura ya ndiyo viti hivyo.
Alisema wananchi hao endapo watafanya hivyo ifikapo Oktoba 25, mwaka huu, watakuwa wamefanya kazi iliyokamilika na watapata maendeleo kwani amani inapatikana mahali ambapo kuna maendeleo. Pia aliwataka wananchi hao kuhakikisha watunza kadi zao za kupigia kura, wasije wakapoteza nafasi hiyo muhimu.
Mama Kikwete aliwataka wananchi hao, kukipa chama hicho kura ya ndiyo kwa sababu kina ilani, ni chama makini na kinafanya kazi kwa mipango.
Akizungumzia kuhusu ilani ya chama hicho,Mama Kikwete alisema,ina mambo makubwa manne, ambayo ni kuondoa umasikini, kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira, kuendeleza vita ya kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Katika uzinduzi huo, Mama Kikwete alimkabidhi vitendea kazi mgombea wa kiti cha Ubunge ,ambavyo ni Katiba ya CCM na ilani hiyo ili aweze kufanya kazi huku akishangiliwa na mamia ya watu walijitokeza uwanjani hapo wengi wao wakiwa ni vijana.
Pia aliwapokea wanachama wapya 12 kutoka Chama Cha Wananchi(CUF) walioongozwa na Laibu Kais, ambaye alikabidhi kadi na bendera ya chama hicho na kuahidi kupeperusha bendera ya CCM kila kata.
Kaisi na waliokuwa wagombea wenzake wa kiti cha Ubunge 10 wameungana ili kumwuunga mkono Kaunje, hatua ambayo ilipongenzwa na Mama Kikwete.
“ Kura zipotosha huwezi kuhama kwenda chama kingine, bali mnaungana na kuwa kitu kimoja ni maneno mazuri ya kuiga mfano,” alisisitiza Mama Kikwete.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Lindi, Mzee Ally Mtopa aliwakemea watu wanaosema kuwa chama hicho hakijafanya maendeleo, ambapo alisema mtu anayesema hivyo, sawa na kumdharau baba yake aliyempeleka shule.
Na Magreth Kinabo-Maelezo,Lindi
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi(NEC) kutoka Zanzibar mkoa wa Mjini, Hadija Hassan Aboud ametoa changamoto kwa wananchi wa wilaya ya Lindi kuhakikisha kwamba wanajitokeza kupiga kura ifikapo Oktoba 25, mwaka huu.
Aidha mjumbe huyo pia ameupongeza mkoa wa Lindi kwa hatua ya maendeleo iliyofikia ukulinganisha na kipindi cha miaka ya nyuma.
Kauli hiyo imetolewa jana jioni na Bi. Hadijah wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chama hicho ya wilaya ya Lindi Mjini iliyoambatana na uzinduzi wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwa lengo la kuinadi , kumnadi mgombea wa kiti cha Urais Dkt. John Magufuli na Ubunge ,ikiwemo kuwanadi wagombea wa viti vya udiwani ,iliyofanyika kwenye uwanja wa Fisi.
“Ninawaomba mjitokeze kupiga kura siku ya kupiga kura, kwani ni siku muhimu, mgombea hawezi kushinda usipopiga kura.Kura moja inathamani. Sisi kwetu siku ya kupiga kura hakuna kulima hata mgonjwa… anachukuliwa ili aweze kupiga kura. Kura moja ni mali,” alisema Bi. Hadijah.
Bi . Hadijah Aliongeza kwamba wajitokeze kukipigia kura chama hicho, ili nchi ya Tanzania iendelee kuwa na amani.
Mjumbe huyo alialikwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi(NEC) wa Wilaya ya Lindi , kwenye uzinduzi huo ,alisema Lindi anayoifahamu siyo aliyoikuta.
“Zamani ukitoka Dares Salaam saa 11:00 asubuhi unafika Lindi saa 3:00 usiku huku uso ukiwa na vumbi. Leo ukitoka Dar es Salaam saa 11:00 asubuhi unafika Lindi saa 5:00 asubuhi bila uso kuwa na vumbi. Maendeleo yaliyoko Lindi ni mafanikio na matunda ya utekelezaji wa Ilani ya CCM,” alisisitiza.
Bi. Hadijah akizungumzia kuhusu Ilani ya CCM ya sasa alisema katika ukurasa wa 71 imeonyesha kwamba kiwanja cha ndege kitafanyiwa marekebisho na kujengwa upya na kimepewa kipaumbele.
Alifafanua kuwa katika ukurasa wa 115 hadi 118 imeonyesha kuwa shughuli za vijana,wanawake,wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo na wakubwa wataendelezwa, afya pia imo, yakiwemo mambo mengi.
Hivyo aliwataka wananchi hao kuwachagua wagombea hao ili chama hicho kiweze kupata ushindi wa Tsunami.
No comments:
Post a Comment