Hussein Makame-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP
Ernest Mangu kuwahamishia Utumishi baadhi ya wafanyakazi wa jeshi hilo ambao si
askari ili kujenga nidhamu ya kijeshi katika wizara hiyo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo Ikulu
jijini Dar es Salaam, mara baada ya kushuhudia kiapo cha uadilifu kwa viongozi
wa umma kwa askari 58 wa jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo hivi karibuni. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Alilazimika
kutoa agizo hilo kufuatia tukio la kusimamishwa kazi kwa Mhasibu Mkuu
wa Jeshi la Polisi, Frank Charles Msaki kutokana na tuhuma za kufanya malipo
hewa huku akidaiwa kutumia madaraka yake vibaya.
“Wahamishieni
kule Utumishi wale wakorofi ili hawa raia wanaofanya kazi kwenye nafasi za
jeshi waondoke, kwani hakuna askari wanaojua masuala ya fedha? Huwezi ukachanganya
askari na wafanyakazi wasio askari.Naomba IGP uliangalie vizuri hili ili raia
ambao wanasumbua jeshi uwapeleke Utumishi” alisema Rais Dkt. Magufuli.
Akifafanua kuhusu mhasibu aliyesimamishwa,
Rais Magufuli alisema mhasibu huyo alikuwa na mamlaka hata ya kuwakemea askari,
ndipo alipotoa agizo asimamishwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amemuagiza
IGP kufuatilia taarifa inayodai kuwa kuna mfanyabiashara aliyelipwa mabilioni
na Jeshi hilo bila ya kutoa huduma ya kushona sare za askari.
Alisema taarifa za mfanyabiashara huyo
zinadai kuwa alilipwa kati ya Shilingi bilioni 20 hadi 60 bila ya kutoa huduma
hiyo, huku jeshi la Polisi likiwa halijatoa taarifa yoyote kuhusu madai hayo.
Alisema wakati fedha hizo zikidaiwa
kulipwa bure, fedha hizo zingeweza kusaidia jeshi hilo kulipia kodi magari yake
77 yanayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pamoja na maagizo hayo, Rais Dkt.
Magufuli alieleza kuridhishwa na utendaji kazi wa jeshi hilo na kueleza kuwa
kutokana na hali hiyo aliona ni wajibu
wake kuwapandisha vyeo askari ambao utendaji kazi wao ni wa kuridhisha.
Hata hivyo alisema alilazimika kuyaondoa
majina ya askari 17 kati ya askari 60 waliopandishwa cheo cha Kamishna Msaidizi
Mwandamizi (6) na Kamishna Msaidizi wa
Polisi (11) kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wao.
Aliwataka makamanda hao wa Jeshi la
Polisi kuhakikisha hakuna wafanyakazi hewa kwenye maeneo yao ili fedha
zinazotumika kulipa wafanyakazi hao zitumike kuboresha maslahi ya askari wa
jeshi hilo.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba aliwataka askari waliopandishwa cheo kwenda kushughulikia
matatizo ya wanyonge badala ya kuwashughulikia wanyonge waliopo kwenye maeneo
yao ya kazi.
Alisema changamoto kubwa iliyo mbele
yao ni kuhakikisha wanakomesha vitendo vya wananchi kuchukua sheria mikononi
kwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na uadilifu na hivyo
kuthibitisha uwezo wao kwa Rais aliyewapandisha cheo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Maadili
Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema askari waliokula kiapo cha uadilifu
wanapaswa kuthibitisha kiapo hicho kwa kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia
vizuri amana za Serikali na kuzingatia maadili ya utumishi na uzalendo.
Aliwataka makamanda wa Polisi
kuhakikisha kunakuwepo kamati za maadili katika maeneo yao kuanzia ngazi za
wilaya na mikoa ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia maadili
na uadilifu.
Kwa upande wake, IGP Mangu
alimuhakikishia Rais Dkt. Magufuli kuwa askari wa jeshi hilo wanazingatia
maadili ya kazi yao na kwamba pale watakapokengeuka atawachukulia hatua mara
moja.
Alisema kati ya askari 60
walipondishwa cheo, askari wawili Juma Abdul Yusuph na Modestus Lyimo
wameshindwa kuhudhuria kiapo hicho kutokana na kuhudhuria mafunzo ya kuwajengea
uwezo wa kazi zao nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Mstaafu Projestus Rwegasira aliwataka askari
waliopandishwa vyeo wahakikshe wanawasimamia askari walio chini yao ili
watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia kipato hicho, Kamanda wa
Polisi mkoa wa Tanga ambaye amepandishwa cheo cha Naibu Kamishna wa Polisi, ACP
Leonard Paulo aliahidi kutekeleza majukumu yake ikiwemo kusimamia askari walio
chini yake kwa kuzingatia maadili.


No comments:
Post a Comment