Na. Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ameunda Kamati
ya wajumbe kumi itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt.
Hassan Abbasi, kuchunguza ufanisi katika mkataba baina ya Shirika la Utangazaji
la Taifa (TBC) na Kampuni ya Star Times.
Taarifa
iliyotolewa leo na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo inaeleza kuwa mbali na Dkt. Abbasi, wajumbe wengine wanaunda
Kamati hiyo kutoka upande wa Tanzania ni Bw. Kyando Evod kutoka Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Frederick Ntobi na Injinia James
Kisaka wote kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Bw. Mbwilo
Kitujime kutoka TBC.
Aidha,
taarifa hiyo imeeleza kuwa majina ya wajumbe wengine watano walioteuliwa kutoka
upande wa China yatawasilishwa ili kukamilisha idadi ya wajumbe kumi wa Kamati
hiyo.
“Kamati
imepewa hadidu za rejea takribani nane na inatakiwa kufanya kazi kwa muda wa
siku saba kukamilisha kazi hiyo”, inaeleza taarifa hiyo.
Kamati
hiyo imeundwa kufuatia kutopatikana kwa faida kwa kipindi cha miaka saba sasa
katika mkataba baina ya TBC na Kampuni ya Star Times.
Kabla
ya kuunda Kamati hiyo, jana Waziri Mwakyembe alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni
ya Star Times kutoka China, Xinxin Pang kujadiliana kwa kina juu ya mkataba huo
ambapo katika majadiliano hayo walikuwepo wafanyakazi wa Wizara hiyo akiwemo
Katibu Mkuu, Profesa Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) Dkt. Abbasi.
Sakata
la mkataba baina ya TBC na Star Times lilichukua sura mpya baada ya Rais Dkt.
John Pombe Magufuli kutembelea ofisi za TBC mwezi Mei mwaka huu na kuonesha
kukerwa na kutopatikana kwa faida katika mkataba huo kwa kipindi cha miaka saba
na kuagiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki.
No comments:
Post a Comment