Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema Myeya, akimkaribisha Mkuu wa Chuo cha Ujenzi, Morogoro Bw. Melkzedeck Mlyapatali, kufunga semina elekezi kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake kutoka mikoa yote ya Tanzania bara, mkoani Morogoro.
Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Ujenzi, Morogoro Bw. Melkzedeck Mlyapatali, akifunga semina elekezi kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara kutoka mikoa yote ya Tanzania bara (hawapo pichani), iliyokuwa na lengo la kuwajengea ujuzi, uwezo na njia mbadala za kuongeza idadi ya wanawake katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, mkoani Morogoro
Baadhi ya waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara kutoka mikoa yote ya Tanzania bara wakifurahi jambo wakati wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Chuo cha Ujenzi, Morogoro Bw. Melkzedeck Mlyapatali, wakati akifunga semina elekezi iliyoandaliwa na Wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), na kufanyika katika ukumbi wa chuo hicho mkoani humo.
Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Ujenzi, Morogoro Bw. Melkzedeck Mlyapatali (kulia aliyekaa kwenye kiti) akiwa na waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara kutoka mikoa yote Tanzania bara, mjini Morogoro. Pembeni yake ni Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema Myeya.
*********************************
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano imesema itahakikisha wanawake walio katika Sekta ya Uhandisi na
Ukandarasi wanapata fursa za kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya
ujenzi na matengenezo ya barabara.
Hatua hii inalenga
kuongeza ushirikishwaji wa wanawake katika sekta hiyo ili kufikia lengo la kuwa
na uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza mkoani
Morogoro, wakati wa ufungaji wa semina elekezi kwa waratibu wa mikoa wa ushirikishwaji wa wanawake
katika kazi za barabara kutoka ofisi za Wakala wa Barabara (TANROADS), mikoa yote Tanzania bara, Mkuu wa Chuo cha Ujenzi,
Morogoro Bw. Melkzedeck Mlyapatali, amewashauri kuwa mabalozi wazuri wa
kuwahamasisha na kuelimisha wanawake katika maeneo yao ya kazi kuchangamkia
fursa hizo.
Aidha amewaasa waratibu hao kuhakikisha wale
wanawake ambao tayari wamefanikiwa kupata kazi
hizo zifanywe kwa kuzingatia ubora, gharama nafuu na kuzingatia muda
uliopangwa kwenye mkataba.
Bw. Mliyapatali ametumia fursa hiyo kutoa wito
na kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao hususan wa kike katika Vyuo vya
Ufundi ili kupata ujuzi wa masuala ya Ujenzi utakaosaidia kuondoa dhana kuwa
masomo ya ufundi ni kwa ajili ya watoto wa kiume tu.
"Mimi pia ni mwalimu hapa chuoni, kwa
uzoefu wangu nimegundua kuwa ukimfundisha mtoto wa kike anakuwa mahiri na
weledi wa hali ya juu, tofauti na mtoto wa kiume", amesema Bw. Mlyapatali.
Kwa upande wake Mratibu wa kitengo cha
ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Rehema Myeya, amewahimiza waratibu
walioshiriki semina hiyo kutoka Mikoa mbalimbali kuwa chachu ya maendeleo
katika vituo vyao vya kazi na kuhakikisha kuwa wanawake watakaopata kazi za
ujenzi au matengenezo ya barabara zinakuwa katika viwango vinavyokubalika.
Naye Mratibu kutoka Wakala wa Barabara Nchini
(TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Prisilla Mushi, ameahidi kusimamia,
kuelimisha, kuhamasisha na kutoa msukumo kwa jamii katika ushiriki wa wanawake
kwa kutumia teknolojia katika kazi za barabara.
No comments:
Post a Comment