Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Afisa Mtetezi CCBRT Bw. Fredrick Msigala kwenye viwanja vya Bunge baada ya kuwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019, bungeni mjini Dodoma leo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
**********************************************************
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa watu
wenye ulemavu kwa kuzingatia sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kusimamia uundwaji
wa kamati zinazoshughulikia masuala yao hapa nchini.
Ameyasema
hayo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) wakati akiwasilisha hotuba ya mapitio na
mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za
ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Bungeni dodoma.
Amesema
Serikali itaboresha mazingira ya watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha uundwaji wa
kamati zao zinazotambulika kisheria ili kusaidia kutatua changamoto
zinazowakabili na kuhakikisha kila mkoa unaunda kamati hizo ambapo hadi sasa
mikoa 12 imekamilisha zoezi la uundwaji wa kamati hizo.
“Tayari
Serikali imeunda kamati za watu wenye ulemavu katika mikoa 12 ya Geita, Kagera,
Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Singida, Rukwa, Shinyanga, Simiyu na
Tabora. Ufuatiliaji unaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa mikoa mingine
nayo inaunda kamati hizo,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu amesema katika kuhakikisha uboreshaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu,
Serikali imeendelea kutoa vifaa zaidi ili waweze kushiriki katika shughuli za
kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi.
“Serikali
kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa vifaa saidizi kwa jamii ya watu
wenye ulemavu ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila utegemezi kwa kuwapatia
baadhi ya vifaa ikiwemo viti mwendo 240, bajaji 6, magongo ya kutembelea 350,
kofia pana 128, fimbo nyeupe 175, miwani maalum kwa wenye uoni hafifu 70, shime
sikio 20, vyerehani 8, vifaa vya kukuzia maandishi 65, mafuta maalum ya kukinga
ngozi dhidi ya mionzi ya jua 35, viti maalum vya kuogea 50 na nyenzo nyingine
za kujimudu,” alisema.
Alisema
Serikali imeendelea kuviboresha vyuo vya watu wenye ulemavu vya Yombo, Dar es
Salaam na Sabasaba, Singida ili kuhakikisha wanashiriki katika fursa zote
ikiwemo za elimu ili wawe na ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika fursa za
ajira nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sheria Na. 9 ya Watu Wenye Ulemavu ya
mwaka 2010.
Alisema
Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na
kukamilisha uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo wa Watu wenye Ulemavu,
kuanzisha madawati ya watu wenye ulemavu, kuhamasisha sekta binafsi na umma
kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu na kuwataka waajiri wote wawaajiri
watu wenye ulemavu wenye sifa kwenye nafasi mbalimbali.

No comments:
Post a Comment