Habari za Punde

TRA YAJIVUNIA KUONGEZEKA KWA MAPATO MIAKA MINNE YA JPM

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Msafiri Mbibo akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya TRA katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
******************************************
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kuongeza mapato ya Serikali kipindi cha miaka minne kutoka 2016 hadi 2019 kwa jumla ya shilingi trilioni 58.3 ikilinganiswa na miaka minne iliyopita ambapo ilikuwa shilingi trilioni 34.97.
Kwa miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, TRA imekuwa ikikusanya wastani wa shilingi trilioni 1.3 ikilinganishwa na wastani wa shilingi bilioni 850 kabla ya awamu ya tano haijaingia madarakani.
TRA imesema kuwa, kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba mwaka huu, wastani wa makusanyo umeweza kupanda na kufikia kiasi cha shilingi trilioni 1.45 kwa mwezi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Msafiri Mbibo alisema kuwa, mafanikio hayo yametokana na msukumo wa serikali ya awamu ya tano ya kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
"Mafanikio haya yanatokana na msukumo wa serikali ya awamu ya tano kuendelea kuboresha mikakati ya ukusanyaji wa mapato, kuibua vyanzo vipya vya kodi pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano wa TRA wa ukusanyaji wa kodi wenye dhamira ya kuongeza makusanyo ya kodi za ndani ikiwemo kukuza ulipaji kodi wa hiari," alisema Mbibo
Mbibo alisema kuwa, sababu nyingine ya kuongezeka kwa makusanyo hayo ni pamoja na kuimarika kwa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD) badala ya stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono. 
"Mafanikio hayo yametokana pia na uhamasishaji wa Mashine za EFD pamoja na kuboresha mifumo ya makusanyo yanayoendana na mazingira ya sasa ya ukuaji wa sayansi na teknolojia ili kuhakikisha walipa kodi wanalipa kwa urahisi kama ilivyo dhamira ya kurahisisha ulipaji kodi na kufanya mazingira kuwa bora," alibainisha Mbibo. 
Mbibo aliwapongeza wafanyabiashara wote walioitikia wito wa Serikali kwa kutumia Mashine za Kielektroniki za EFD bila kuwasahau wananchi ambao wamekuwa wakidai risiti kila wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.
Naibu kamishna Mkuu huyo alizungumzia mafanikio mengine kuwa ni ongezeko la mizigo kutoka nje ya nchi kupitia bandari za Dar es Salaam na udhibiti wa makusanyo ya bidhaa zinazopaswa kulipiwa kodi na ushuru ziendazo nje ya nchi mfano zao la korosho na mazao ya ngozi na kwato.
Pia, mwezi Juni mwaka 2018 TRA ilianzisha Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki ulioanza kutumika rasmi Januari 15 mwaka huu ambao ni mbadala wa stempu za karatasi za kubandika ambazo zilikuwa zikitumika hapo awali.
Alifafanua kwamba, lengo la kuanzisha mfumo huo mpya ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na ushuru wa bidhaa, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Mapato pamoja na kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ya kutokutendewa haki ya makadirio ya kodi zinazosimamiwa na TRA. 
"Kutokana na utekelezaji wa mfumo huo kwenye eneo la pombe kali na mvinyo tu, TRA imekusanya ushuru wa bidhaa sh. bilioni 77.8 kwa kipindi cha mwezi Februari hadi Oktoba, 2019 ukilinganisha na kiasi cha sh. bilioni 58.2 kilichokusanywa kipindi kama hicho mwaka jana," alisema Mbibo.  
Mbibo aliongeza kuwa, "Kwa upande wa bidhaa za vinywaji laini yaani soda na vinywaji vingine visivyo vya kilevi ambapo matumizi ya mfumo huo yalianza Agosti, 2019, kwa mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu, TRA ilifanikiwa kukusanya sh. bilioni 10 ukilinganisha na sh. bilioni 9.2 zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka uliopita".  
Msafiri Mbibo ameeleza kuwa ni matumaini ya TRA kuwa jinsi mfumo huo utakavyoimarika na jamii kutambua unavyofanya kazi na umuhimu wake ndivyo mapato yatakavyoongezeka.  
Mamlaka ya Mapato Tanzania ni taasisi ya Serikali ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.11 ya mwaka 1995 na ilianza kufanya kazi tarehe 1 Julai, 1996 na moja ya majukumu yake makuu ni kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya Serikali.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.