Habari za Punde

HATIMAYE TRENI YA DAR-MOSHI YAANZA RASMI BAADA YA MIAKA 25

 Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, TRC Amina Lumuli (wa nne kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA Mhandisi Dk. John Ndunguru, wakiinua na kupeperusha bendera ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa safari ya Treni ya Dar es Salaam-Moshi iliyoanza leo. Treni hiyo itakuwa ikifanya safari zake mara mbili kwa wiki ambapo Dar itakuwa ni siku ya Jumanne na Ijumaa wakati Moshi itakuwa ni Jumatano na Jumamosi. (Picha an Muhidin Sufiani).
****************************************
Na Dina Mgana
HATIMAYE ndoto ya kutumia usafiri wa treni katika ukanda wa kaskazini imerejea tena baada ya garimoshi kutoka Dares Salaam kwenda Moshi, kuanza safari zake rasmi jana.
Treni hiyo iliyanza kufanya safari zake kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Moshi, imezinduliwa jana huku ikianza na jumla ya Mabehewa tisa na Injini mbili.
Akuzungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo Mhandisi Dk. John Ndunguru, ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi LATRA, alisema reli hiyo ilikufa kwa miaka 25 iliyopita, hivyo kupitia uzinduzi huo itasaidia wananchi wa Kanda ya Kaskazini kutopata changamoto ya usafiri.
“Kwanza tunaishukuru serikali ya awamu ya tano, kwa kuthubutu kufufua reli hii iliyokua imekufa kwa takribani miaka 25, iliyokuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, hata hivyo tunaamini changamoto ya abiria kukosa usafiri sasa itakwisha” alisema Mhandisi Ndunguru.
Alisema usafiri huo utaondoa tatizo la kupandishwa nauli bila kufuata utaratibu na hasa nyakati za  mwisho wa mwaka kama ilivyo kwa mabasi yanayofanya safari za kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, kwani abiria wengi watakua wakitumia treni ambayo ni usafiri wa uhakika zaidi na wenye bei nafuu.
Aidha alisema kuwa utaratibu uliowekwa kwa sasa utakuwa na usimamizi wa kutosha katika kusimamia tiketi zinazokatwa kuwa sawa na abiria wanaosafiri, kwani tiketi zote zitakuwa zikikatwa kwa njia ya kielektroniki ili kuepusha usumbufu na ajari zisizo za lazima kutokana na kujaza abiria kuzidi uwezo wa treni.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli Tanzania TRC,  Amina Lumuli,  alisema treni hiyo itakuwa ikifanya safari zake mara mbili kwa wiki, ambapo kwa upande wa Dar es Salaam itakuwa jumanne na Ijumaa wakati kwa upande wa Moshi itakuwa ni jumatano na jumamosi.
Aliongeza kuwa njia za Reli ya kati zimeimarishwa, ikiwa ni pamoja na wakaguzi wa treni kupita kukagua njia yote kabla ya treni kuanza safari.
“Tunawaomba wananchi wawe mstari wa mbele katika kulinda miundombinu ya hiyo kwani reli ni yetu sote na treni ni ya Watanzania wote.” Alisema Amina.
Alisema wananchi wawe mabalozi wazuri katika ulinzi wa miundombinu ya reli kwa kufanya hivyo kutaondoa hujuma na changamoto zinazoweza kujitokeza ili kuharibu miundombinu hiyo.
Vilevile aliwashukuru wananchi waliojitokeza kwaajili ya kutumia usafiri huo kwa mara ya kwanza baada ya kukwama kwa miaka mingi, ambapo alisema abiria waliokata tiketi ni wengi na treni imeondoka ikiwa imejaa siti zote.
Kelvin Mosha mmoja wa wasifiri alisema anaishukuru serikali kwa kuzindua reli hiyo, kwani itakuwa msaada mkubwa kwao kwakutopata changamoto ya usafiri kama ilivyokuwa awali.
“Kwa kweli tunaishukuru serikali yetu kwakuturejeshea usafiri wa reli ya kati ambao tuliukosa kwa miaka mingi kwa sasa naona utaturahisishia na hasa kuelekea kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya. Alisema Mosha
Naye mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Rajab Athuman, alisema kuwa kwa upande wake usafiri huo utawarahisishia usafirishaji wa mizigo ambayo utakuwa ni bei nafuu na uhakika wa safari kwa mizigo yao.  
 Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, TRC Amina Lumuli (wa tatu  kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA Mhandisi Dk. John Ndunguru, baadhi ya viongozi wakipunga mikono kuwaaga abiria wakati wa uzinduzi rasmi wa safari ya Treni ya Dar es Salaam-Moshi iliyoanza. Treni hiyo itakuwa ikifanya safari zake mara mbili kwa wiki.
 Baadhi ya wananchi wakishuhudia usafiri huo wa Treni.

Baadhi ya abiria wa kwanza waliosafiri na Treni hiyo.
 Baadhi ya abiria wa kwanza waliosafiri na Treni hiyo.
 Picha ya pamoja ya baadhi ya Viongozi wa TRC

Abiria waliosafiri na Treni hiyo wakipunga mkono kuaga ndugu zao. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.