Habari za Punde

WYDAD VS SIMBA KUCHEZESHWA NA MWAMUZI ALHADI ALLAOU KUTOKA CHAD, KOCHA SIMBA AKIRI KUKUTANA NA MECHI NGUMU

Kocha Mkuu wa Simba Sports Club, Roberto Oliviera maarufu Robertinho amekiri kuwa mechi dhidi ya  Wydad kuwa ni ngumu na kuahidi kupigana kufa na kupona ili kufuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba imeondoka nchini jana Jumatatu usiku kuelekea Casablanca tayari kuumenyana na Wydad siku ya Ijumaa kwenye uwanja wa Mohammed V, Casablanca.
Simba inahitaji sare yeyote ili iweze kufuzu hatua inayofuata ya michuano hiyo kufuatia ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya awali kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi iliyopita.
Robertinhno alisema wanajua ni kazi kubwa watakayokutana nayo katika mchezo huo kwani wanapambana na timu ambayo ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo.
AAidha aisema kuwa wachezaji wake wanafahamu umuhimu wa mechi hiyo na wako tayari kukabiliana na changamoto kutoka kwa wapinzani wao.
“Ni dhahiri tunakwenda kukabiliana na hali ngumu nchini Morocco, lakini hili ni soka na hata Wydad wanajua jinsi Simba ilivyo imara. Pia wanazungumza juu yetu.
Wachezaji wangu wako tayari kwa mapambano. Njia yeyote ya mafanikio ni ngumu na inahitaji kupigana kiume. Lengo letu ni kuwaondoa Wydad na timu nyingine ambazo tutakutana nazo,” alisema Robertinho.
Nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Hussein almaarufu Tshabalala alisema wachezaji wameadhimia kupambana kiume na kujituma ipasavyo siku ya mchezo huo ili kupata matokeo yenye faida kwa na bora katika mchezo wa marudiano.
Alisema wamejiandaa vyema kabla ya pambano hilo na kazi kubwa iliyo mbele yao ni kuwapa Watanzania kile wanachokitarajia.
"Tulicheza dakika 90 za kwanza kwenye uwanja wetu wa nyumbani na tutacheza dakika 90 nyingine ugenini. Haitakuwa mechi rahisi kwa sababu hata Wydad pia wanamalengo sawa na sisi, na hawatakubali kukubali kudhalilika kwao hivyo tutapigania klabu yetu na nchi yetu pia,” alisema Tshabalala.
Alieleza kuwa Wydad ni timu yenye nguvu na hakuna haja ya kuwa na wasiwasi badala yake wanatakiwa kujituma na kucheza kwa kujihami muda wote.
Mshindi wa mchezo huo atakutana na mshindi kati ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Chabab Belouizdad ya Algeria. Katika mechi ya kwanza, Mamelodi Sundowns ilishinda 4-1 ugenini.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi kutoka nchini Chad, Alhadi Allaou Mahamat, ambaye atasaidiwa na  Elvis Guy Noupue Nguegoue wa Cameroon na Issa Yaya wa Chad pia. Mwamuzi wa akiba ni Mahmood Ali Mahmood Ismail wa Sudan.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.