“Kili Taifa Cup toe vipaji vya Ligi Kuu Tanzania Bara”
KUMALIZIKA kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ndiyo mwanzo wa michuano ya Kombe la Taifa ambayo kwa mwaka wa nne sasa ipo chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro.
Awali TBL imekuwa ikidhamini michuano ya Taifa Cup kwa miaka miwili mfululizo kupitia bia yake ya Safari Lager kabla ya kuhamishia kwa bia ya Kilimanjaro ambao huu utakuwa mwaka wa pili mfululizo.
Michuano hii ambayo imebatizwa jina la Kili Taifa Cup huandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TFF Fredrick Mwakalebela, michuano hii ni kongwe kuwahi kuandaliwa na shirikisho hilo (zamani ikijulikana kama FAT-Chama cha Mpira wa Miguu). Aidha kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Taifa Cup, michuano hii ilikuwa inafahamika kama Sunlight Cup.
Historia inaonyesha kuwa Taifa Cup ilifutwa mwaka wa 1997 kutokana na ukosefu wa udhamini. Hata hivyo udhamini wa TBL kuanzia mwaka wa 2005 na hususan baada ya Leodegar Tenga kuchaguliwa rais wa TFF, michuano ya Taifa Cup ikafufuliwa.
Ni dhahiri kuwa wachezaji wengi wazuri enzi hizo waliibuka katika michuano ya Taifa Cup ukiachilia mbali mashindano katika shule maarufu kama UMETASHUMTA na UMISETA.
Huku tukisubiri kuanza kwa Kili Taifa Cup Mei 8 ambayo katika hatua za awali itachezwa kwa kanda sita ambazo ni Mwanza, Arusha, Dodoma, Iringa, Tanga na Mtwara, ni vyema pia makocha na si uongozi wa klabu wakatupia macho michuano hii ili kupata wachezaji bora wakuwasajili.
Ninasema makocha ni si viongozi wa klabu kwasababu jukumu la kusimamia usajili lipo chini ya mwalimu. Kosa kubwa ambalo klabu nyingi zetu zinafanya ni uongozi kumchagulia mwalimu wachezaji. Na wakati mwingine humpangia kikosi mwalimu mpaka inabidi mtu ujiulize, kwanini kuajiri kocha?
Hivi karibuni aliyekuwa kocha wa timu ya Moro Unitied ambayo imeshuka daraja, Juma Mwambusi, alinukuliwa na vyombo vya habari akilalamika kuwa uongozi ulikuwa unampangia kikosi. Kimsingi, uongozi unavuka mpaka kwasababu kazi yao ni kutawala na kusimamia maendeleo ya klabu wakati kocha ambaye ni mtaalamu anajukumu la kuwanoa wachezaji na kutengeza kikosi kilicho imara.
Hivyo basi ni bora kama uongozi utamwachia mwalimu jukumu la kusajili wachezaji ambao wanamfaa kwa Ligi Kuu Bara msimu ujao. Na kazi hii ianze kwa michuano ya Kili Taifa Cup. Uzuri wa michuano hii ni kwamba wachezaji kutoka takribani mikoa yote ya Tanzania Bara wanapata fursa ya kuonekana na kuonyesha vipaji vyao.
Kama makocha na hususan wanaonoa miamba ya soka nchini watayatumia vizuri Kili Taifa Cup, bila shaka tutaepukana na wimbi la kusajili wachezaji kutoka nje. Si vibaya kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi hasa ukizingatia wale bora huleta chachu ya ligi na kuipandisha chati ligi yetu, lakini kuna vipaji vingi humu humu ambazo kama klabu tunashindwa kuviendeleza.
Wachezaji ambao wanaibuka katika michuano kama hii ya Kili Taifa Cup na kupata kusajiliwa katika klabu zetu za ligi kuu huku vipaji vyao vikiendelezwa, wanauwezo wa kuuzika nje ya nchi na kucheza soka la kulipwa.
Lengo kubwa la kuanzishwa Kili Taifa Cup ni kutambua vipaji vipya katika medani ya soka na kisha kuviendeleza. Ila ni mara chache sana hususan katika miaka ya hivi karibuni kwa wachezaji nyota wanaoibuka baada ya michuano ya Kili Taifa Cup kupata nafasi katika klabu za ligi kuu.
Ni matumaini ya wadau wengi wa soka kwamba makocha na hasa wale wa ligi kuu watayafwatilia kwa makini michuano hii ya Kili Taifa Cup na kuingia katika ushindani wa usajili wachezaji bora watakaoibuka.
Kili Taifa Cup ambayo inaanza Mei 8 hadi 30 chini ya udhamini wa TBL kwa kiasi cha shilingi milioni 850, licha ya kunyanyua viwango vya wachezaji, pia hufufua hamasa mikoani. Michuano hii ni ya mikoa. Zamani wenyeji wa mikoa husika walikuwa wanajitokeza kwa wingi kushangilia timu zao. Wachezaji nao walikuwa wakirudi kuwakilisha mikoa yako.
Hayo yote yamebadilika sasa kwani mchezaji halazimishwi kuwakilisha mkoa wake. Ila kwa upande wa mashabiki, hamasa inaonekana kuwa kubwa. Aidha Kili Taifa Cup huleta ushindani ukizingatia wakuu wa mikoa ni walezi wa mikoa zao husika.
TFF wamepanga vituo sita kutoka sehemu mbalimbali nchini kutumika wakati wa awali ya michuano hiyo huku robo fainali hadi fainali ikihamishwa Dar es Salaam. Hii inamaanisha kuwa mashabiki wengi mikoani watapata fursa ya kushuhudia baadhi ya mechi katika hatua za awali za michuano hiyo huku pia wenye bahati wakijishindia vifurushi vya zawadi kutoka kwa mdhamini, TBL, ambao watakuwa wakifanya promosheni.
Labda siku za usoni ni vyema kama Kili Taifa Cup ikarudia enzi zake za zamani ambapo timu zingecheza nyumbani na ugenini. Hii itawapa hamasa zaidi mashabiki na kuwapa fursa zaidi kuziona na kushabikia timu zao.
TBL tayari wameweka hadharani zawadi za washindi ambapo mshindi wa Kili Taifa Cup mwaka huu atajinyakulia shilingi milioni 35 huku mshindi wa pili akijizolea shilingi milioini 20 na watatu shilingi milioni 10. Aidha kocha bora, mwamuzi bora, mchezaji bora, timu yenye nidhamu na mfungaji bora kila moja atapewa shilingi milioni mbili.
Ni matumani ya wadau wengi wa soka kwamba mchezaji na mfungaji bora wa michuano ya mwaka huu atasajiliwa na mojawapo ya timu za ligi kuu ili vipaji vyao viendelezwe.
No comments:
Post a Comment