Habari za Punde

*NANI KUKOSA FAINALI ZA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA.

IMEELEZWA kuwa winga machachari wa timu ya Manchester United, Nani ameondolewa katika kikosi cha timu ya Taifa cha Ureno kitakachoshiriki kwenye fainali za Kombe la dunia zinazotaraji kuanza juni 11 mwaka huu.
Maelezo yaliyotolewa na mtandao wa Shirikisho la soka la nchini Ureno yalieleza kuwa “Kutokana na uchunguzi wa vipimo imeonekana kuwa, Nani, hatoweza kucheza soka la ushindani katika fainali hizo na taarifa za kidaktari zitawakilishwa katika idara ya afya ya klabu ya Manchester United”.
Aidha taarifa za nyota huyo wa Kireno juu ya kukosa fainali za michuano ya kombe la dunia zitakazofanyika Afrika ya kusini, zimetangazwa leo baada ya mchezaji huyo kupata majeraha ya mfupa wa bega, siku ya Ijumaa iliyopita wakati akiwa kwenye mazoezi.
Kwa hatua hiyo sasa nafasi ya Nani, itachukuliwa na kiungo wa Benfica, Ruben Amorim.
Kukosekana kwa winga huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye kwa hakika ndiyo kwanza ameanza kupata mafanikio na umaarufu mkubwa katika dimba la Old Trafford, huenda kukavuruga mipango ya kocha wa Ureno, Carlos Queiroz, aliyekuwa akimtegemea zaidi winga huyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.