Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Naibu Mhariri Mtendaji wa kampuni ya New Habari (2006) Bw. Danny Mwakiteleko aliyefariki usiku wa kumkia Jumamosi.
Mwakiteleko ambae pia alikuwa Mhariri Mkuu wa habari wa gazeti la RAI linalochapishwa na New Habari (2006)amefariki dunia katika taasisi ya Mifupa ya hospitali ya taifa Muhimbili - MOI alikofikishwa na kufanyiwa upasuaji wa kichwa kufuatia ajali ya gari aliyoipata katika barabara ya Mandela eneo la Tabata jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia Jumatano wiki iliyopita.
Vodacom imeguswa na kifo chake katokana na ukweli kwamba Danny ni mmoja wa waandishi wa habari mahiri waliokuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya habari akiongozwa na sifa za ucheshi,uchapakazi, kujituma, ubunifu, na mwenye kutoa ushirikliano kwa wanahabari wenzake wakati wowote.
Kazi za Marehemu Mwakiteleko alizozifanya wakati wa uhai wake kupitia Magazeti ya Majira,Mwananchi na Magazeti ya New Habari (2006) zitaendelea kukumbukwa na kila mmoja ambapo kupitia maandiko yake wananchi na wadau mbalimbali wamenufaika kwa kuelimika na kuhabarika.
Vodacom ikiwa ni kampuni inayojali na kuheshimu kazi na taaluma ya uandishi wa habari na wanahabari wenyewe inatoa rambirambi kwa familia ya marehemu Mwakiteleko, Kampuni ya New Habari (2006), Jukwaa la wahariri, Umoja wa wamilki wa vyombo vya habari - MOAT, wanahabari,wananchi na wadau wengine wote.
Ni imani yetu kuwa wadau wote wa tasnia ya habari tutaendelea kuwa wamoja na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu tunapoomboleza kifo cha mwenzetu kaka yetu mpendwa Danny Mwakiteleko.
Uongozi na wafanyakazi wa Vodacom upo pamoja na familia ya Marehemu katika kipindi hiki kigumu.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Danny Mwakiteleko mahala pema peponi.
Amin.
No comments:
Post a Comment