Habari za Punde

*ZIMBAMWE WAJIFUA BONGO KUWASUBIRI TWIGA KESHO

 Wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Zimbabwe, wakiwa katika mazoezi ya pamoja kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya mchezo wao wa kesho kati yao na Timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania Twiga Stars, mchezo ubaotarajia kupigwa kesho katika Uwanja wa taifa jijini.
Wachezaji wa Zimbabwe wakiwa mazoezinini jana.



ZIMBABWE YAFURAHIA KUJIPIMA KWA TWIGA STARS
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake ya Zimbabwe imefurahia kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania (Twiga Stars) itakayofanyika Jumamosi (Mei 12 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kocha Mkuu wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza amesema wamefurahi kupata mechi hiyo kwa vile wanaamini Twiga Stars ni kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi yao ya mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria.

Amesema anaijua vizuri Twiga Stars, kwani mwaka jana alicheza nayo mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye nusu fainali ya Kombe la COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare, Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2.

Mechi ya pili ilikuwa kwenye michezo ya All Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo katika mechi yao iliyochezwa Septemba 11 timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Mabao ya Twiga Stars yalifungwa na Asha Rashid na Mwanahamisi Shuruwa.

Mugadza amesema sababu nyingine iliyowafanya watake kucheza na Twiga Stars ni kwa vile ilishacheza na Nigeria kwenye fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010. Twiga Stars ilifungwa na Nigeria mabao 2-1.

Kocha huyo amesema hiyo itakuwa mechi ya pili kujipima nguvu kabla ya kuivaa Nigeria. Mwishoni mwa wili iliyopita Zimbabwe ilicheza mechi ya kirafiki jijini Harare dhidi ya Zambia na kushinda mabao 2-1.

Zimbabwe ambayo iliwasili jana (Mei 9 mwaka huu) saa 1.30 usiku kwa ndege ya South African Airways (SAA) ina msafara wa watu 28 ambapo kati ya hao 20 ni wachezaji wakati waliobaki ni benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo.

Viingilio katika mechi hiyo kati ya Twiga Stars na Zimbabwe itakayochezwa kuanzia saa 10.30 jioni ni sh. 1,000 tu kwa sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh. 10,000 na VIP B ambayo kiingilio chake ni sh. 5,000.

Twiga Stars ilikuwa katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza na inatarajia kurejea kesho (Mei 11 mwaka huu) tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa na mwamuzi wa kimataifa Judith Gamba.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.