RAMBIRAMBI MSIBA WA AMINA SINGO
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa
masikitiko taarifa ya kifo cha aliyekuwa mtangazaji wa habari za michezo katika
kituo cha redio cha 100.5 Times FM, Amina Singo kilichotokea usiku wa kuamkia
jana.
Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa
miguu kwani kwa nyakati tofauti kupitia taaluma ya uhandishi wa habari, Amina
alifanya kazi na TFF, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka
daima.
Tutamkumbuka kama mtangazaji wa habari za mpira wa miguu
na michezo kwa ujumla. TFF tunatoa pole kwa familia za marehemu
Amina Singo, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Amina Singo mahali pema
peponi. Amina
SITA ZATINGA ROBO FAINALI UHAI CUP
Timu sita zimeshakata tiketi ya kucheza hatua ya robo
fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini
ya miaka 20 (U20) wa klabu za Ligi Kuu ya Tanzania.
Hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayofanyika
viwanja vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam na kudhaminiwa na kampuni ya Said
Salim Bakhresa kupitai maji Uhai itafanyika Desemba 19 mwaka huu kwenye viwanja
hivyo hivyo.
Timu zilizofuzu kutoka kundi A ni Coastal
Union ya Tanga, Mtibwa Sugar ya Morogoro na JKT Ruvu ya Dar es Salaam. Kundi C
ni Oljoro JKT ya Arusha na Ruvu Shooting ya Pwani wakati iliyofuzu kutoka kundi
A hadi sasa ni Azam pekee.
Katika mechi zilizochezwa leo asubuhi (Desemba 17 mwaka
huu) Coastal Union na Mtibwa Sugar zimetoka suluhu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume, wakati Uwanja wa Azam ulishuhudia African Lyon ikiifunga Mgambo
Shooting mabao 2-1.
Nafasi mbili za robo fainali zilizobaki kutoka kundi B
zinawaniwa na timu za Simba, African Lyon na Polisi Morogoro. Mechi
itakayochezwa leo saa 10 jioni katika Uwanja wa Chamazi kati ya Polisi Morogoro
na Simba ndiyo itakayoamua timu zitakazoungana na Azam kutoka kundi
hilo.
No comments:
Post a Comment