Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kupigia kura waraka wa
marekebisho ya Katiba, kwani wametimiza wajibu wao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo,
Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba ni jambo muhimu, lakini lazima yapate
ridhaa ya wanaohusika ambao ni wajumbe.
“Nawasukuru wajumbe kwa kupitisha jambo hili.
Nawashukuru wote, waliokubali na waliokataa. Ndivyo demokrasia ilivyo. Tulitaka
waseme ndiyo au hapana, hivyo tulitarajia kupata majibu yoyote kati ya hayo
mawili.
Marekebisho mengine yalikuwa ni maelekezo (directives)
kutoka FIFA na CAF. Katiba yetu inasema tutatekeleza maagizo ya CAF na FIFA,
lakini kwa misingi ya utawala bora tuliona ni lazima tupate ridhaa kutoka kwa
wajumbe,” amesema.
Jumla ya wajumbe waliopiga kura kwa njia hiyo ya waraka
ni 103 ambapo 70 waliunga mkono wakati waliokataa ni 33. Idadi hiyo ni asilimia
68 ya kura zote zilizopigwa, hivyo kupatikana theluthi mbili ya kura zilizopigwa
ili kufanya marekebisho kikatiba.
Vipengele vilivyoingizwa katika marekebisho hayo ni
‘club licencing’ kama ilivyoagizwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF),
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF kama ilivyoshauriwa na Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa
Rais.
Vilevile Kamati ya Utendaji itakutana Desemba 23 mwaka
huu kufanya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi, kutokana na kupitishwa kwa
marekebisho hayo ambayo yanaunda Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF. Pia
itachagua wajumbe wa Kamati ya Rufani ya TFF.
Mkutano Mkuu wa TFF ambapo pia utakuwa na ajenda ya
uchaguzi utafanyika Februari 23 na 24 mwakani. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF,
wajumbe wanatakiwa kupewa taarifa ya Mkutano Mkuu siku 60 kabla.
No comments:
Post a Comment