Mtibwa Sugar ya Morogoro leo asubuhi (Desemba 14 mwaka
huu) imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Toto Africans ya Mwanza katika
mechi ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri
chini ya miaka 20 (U20) za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.
Juma Luzio alifunga mabao yote matatu (hat trick) katika
mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Alifunga mabao hayo dakika za 44,81 na 88.
Hata hivyo, Toto Africans ndiyo walioanza kufunga katika
mechi hiyo ya kundi A. Bao hilo katika michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni
ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai lilifungwa dakjika ya 22 na Pastol
Makula.
Nayo Simba imenguruma baada ya kuitandika Mgambo
Shooting ya Tanga katika mechi nyingine ya michuano hiyo iliyochezwa leo asubuhi
kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi. Wafungaji kwa washindi walikuwa Ramadhan
Mdoe dakika ya 19, Mohamed Salum dakika ya 77 na Ramadhan Singano dakika ya
89.
Michuano hiyo inaendelea leo mchana na jioni. Mechi ya
Ruvu Shooting na Kagera Sugar iliyokuwa ichezwe mchana Uwanja wa Azam, Chamazi
sasa itafanyika saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume.
Mechi nyingine za leo ni Coastal Union vs JKT Ruvu
(mchana- Karume), African Lyon vs Azam (jioni- Chamazi). Vilevile mechi kati ya
JKT Oljoro na Yanga inachezwa leo Uwanja wa Chamazi.
Kesho (Desemba 15 mwaka huu) ni mapumziko, na michuano
hiyo itaendelea Jumapili kwenye viwanja vyote viwili- Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume na Uwanja wa Azam- Chamazi.
No comments:
Post a Comment