CAF KUFANYA UKAGUZI WA ‘LESENI ZA KLABU’ JANUARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litatuma ofisa wake nchini mwezi ujao kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwenye klabu za Ligi Kuu ya Tanzania kabla ya kutoa leseni kwa zile ambazo zitakuwa zimekidhi vigezo vilivyowekwa. Ili klabu ishiriki mashindano ya CAF ni lazima iwe na leseni hiyo.
Kwa mujibu wa CAF, ofisa huyo atakuwa nchini kuanzia Januari 7 mwakani ambapo atafanya ukaguzi huo hadi Januari 14 mwakani. Mbali ya ukaguzi katika klabu, pia ofisa huyo atakagua viwanja vitakavyotumika katika mashindano yake na hoteli ambazo timu kutoka nje zitakuwa zinafikia kabla ya mechi.
Baadhi ya masharti kabla ya klabu kupewa leseni ya CAF ni pamoja na kuwa na ofisi (physical address), uwanja wake wa mazoezi, programu ya maendeleo kwa vijana, sekretarieti ya kuajiriwa, hesabu za fedha zilizokaguliwa (audited accounts) na benchi la ufundi linaloundwa na watu wenye sifa zinazostahili.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA DRFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaupongeza
uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Desemba 12 mwaka huu) hoteli ya
Mbezi Garden.
Ushindi aliopata Almasi Kasongo aliyechaguliwa kuwa
Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji unaonesha jinsi
ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa DRFA walivyo na imani kwao.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya DRFA ambayo hivi sasa ina kinara mpya, na kwamba ina changamoto
kubwa ya kuhakikisha inaendesha shughuli za DRFA kwa kuzingatia katiba na
kanuni.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA chini
ya Juma Simba na Kamati ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa
kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia katiba na
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Safu mpya ya uongozi wa DRFA inaundwa na Kasongo
(Mwenyekiti), Meba Ramadhan (Makamu Mwenyekiti), Msanifu Kondo (Katibu), Muhsin
Said (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF), Benny Kisaka (Mwakilishi wa Klabu),
Ally Hobe (Mhazini) na wajumbe Mohamed Shabani, Sunday Mwanahewa na Bakari
Mapande.
No comments:
Post a Comment