Na Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Watu wanne wa Kundi la “lambalamba”   wanashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani Dodoma  kwa kijifanya wanafichua wachawi katika vijiji mbalimbali katika maeneo ya wilaya za Chamwino, Kongwa na Mpwapwa. kumbe wanawatapeli wanavijiji kwa lengo la kujipatia fedha
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi Bw. David Misime amesema uchunguzi wao umebaini kuwa vitu wanavyojifanya kuvitoa ndani ya nyumba au maduka ya watu, kuwa ni wao wenyewe hutuma wenzao kuvipandikiza na baadaye  hujifanya wamevikuta kwenye nyumba ya mtu anayetuhumiwa kuwa ni mchawi.
Aliwataja waliokamatwa wakiwa wanajiandaa kuendesha shughuli za lambalamba katika kijiji cha Vilundilo Wilayani Kongwa kuwa ni mwanaume mmoja Mkombozi Salehe, na wanawake watatu ambao ni Hadija  Tupa, Joyce  Nhembelo na Siwema  Kwaeli, ambao walikuwa ni kwa ajili ya kuwapikia lambalamba hao.
“Wanawake waengine hutafutwa kwa ajili ya kulala nao jambo ambalo ni hatari kwani mbali ya kwamba ni kinyume cha sheria na unyanyasaji wa kijinsia pia upo uwezekano mkubwa wa kuambukizwa magonjwa ikiwepo UKIMWI.” Alisisitiza Bw. David Misime
Aidha alitoa wito kwa wananchi kuelewa  kuwa wanatapeliwa fedha zao na hao watu waliobuni mradi wa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwani wamejionea wenyewe kuwa wanachangishwa fedha kabla ya kuwaita na hata wanaodaiwa kuwa wachawi, hudaiwa kiasi cha fedha.
Kamanda David Misime alisema kuwa shughuli wanazoendesha kundi hilo la Lamba lamba ni kinyume cha sheria za nchi na ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binanadamu kwa kuwaita baadhi ya watu kuwa ni wachawi kwa lengo la kujipatia fedha.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma alisema Upelelezi zaidi unakamilishwa ili wafikishwe mahakamani wakati wowote, pamoja na  Ufuatiliaji wa lambalamba wengine waliokimbia pamoja na viongozi vijiji wanaoshirikiana nao unaendelea.
Wakati huo huo  Polisi Mkoani Dodoma inamshikilia kwa mahojiano IDDI S/O RAMADHANI PANDAUYAGA @ NGOSHA, MSUKUMA, Mkazi wa DODOMA MAKULU baada ya kulalamikiwa na wananchi wengi kwa kujipatia fedha kwa njia udanganyifu kuwa anawauzia viwanja.
Kamanda Misime amesema hadi sasa mtu huyo ameshatapeli zaidi ya Tshs. 24,537,000/= kuanzia mwezi Agosti, 2012. Kwa kuwarubuni watu kuwa viwanja hivyo ametumwa na wafanyakazi wa CDA kuviuza.
Bw. David Misime alitoa wito kwa wananchi wasikubali kurubuniwa kuwa wanauziwa kiwanja na kutoa fedha bila kuthibitisha kiwanja hicho kama kipo na ni halali.
 
CONTACT:
POLISI MKOA WA DODOMA
DAWATI LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Phone:  0715 006523, Luppy Kung’alo – Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP)
Phone:  0712  360203, Silyvester Onesmo – Police  Konstebo  (PC)

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA